Maonesho ya 44 ya kimataifa ya biashara ya Dar es salaam (44th DITF) yanatarajiwa kufanyika kwa kuzingatia kanuni za afya, ikiwemo mikutano kufanyika kwa mtandao na tiketi kuuzwa kwa simu za mikononi.

Watembeleaji wa ndani na nje ya nchi wa maonesho hayo watapata uwanja mpana kwa kutembelea maonesho hayo kwa kupitia mtandao.

Waziri wa viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa katika taarifa yake kwa umma amesema lengo la maonesho hayo yaliyobeba kaulimbiu “Uchumi wa viwanda kwa ajira na biashara Endelevu” ni kutoa fursa ya kutafuta masoko ya mazao na bidhaa za kilimo, viwanda na huduma nchini.

“Ili kurahisisha utembeleaji wa maonesho, watembeleaji watapata fursa ya kununua tiketi kupitia simu za mikononi. Vilevile watembeleaji kutoka ndani na nje ya nchi watapata fursa ya kutembelea maonesho kupitia mtandao” Amesema Bashungwa

Aidha ametoa wito kwa wafanyabishara, wamiliki wa viwanda vyote nchini, wakulima, taasisi za umma, halmashauri za wilaya na taasisi binafsi kushiriki katika maonesho hayo ili kuongeza wigo wa masoko.

Magufuli atuma shukurani kwa viongozi wadini kwa kupambana na Corona
Wakenya kutotembea usiku kwa siku 30, vita dhidi ya Corona