Katika kutekeleza lengo namba nane la malengo ya maendeleo endelevu SDGs, kuhusu ajira za staha na ukuaji kiuchumi na usawa wa kijinsia, Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo duniani (FAO), nchini Tanzania limezindua tawi la tatu la Mtandao wa Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi TAWFA.

Sherehe za uzinduzi huo, zimefanyika Mkoani Kigoma ambapo Wanawake wavuvi, viongozi wa Serikali na Wafanyakazi wa FAO walifungua rasmi tawi hilo ikiwa ni la tatu baada ya mengine mawili ya awali yaliyozinduliwa kanda ya Ziwa Victoria na Ukanda wa Bahari ya Hindi.

Uzinduzi huo, unafanyika kupitia mradi wa FISH4ACP unaotekelezwa katika Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ambapo Mratibu wa Sekta ya Uvuvi Kitaifa kutoka FAO, Oliva Mkumbo amesema lengo kuu ni kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia uvuvi, ili kuinua kipato cha familia na kuondokana na umasikini.

Mratibu wa Sekta ya Uvuvi Kitaifa kutoka FAO, Oliva Mkumbo (wa tatu kushoto waliokaa) akiwa katika picha ya pamoja na Wanawake wajasiriamali sekta ya Uvuvi Mkoani Kigoma. (Picha na UN)

“Lengo la kuanzisha jukwaa la wanawake ni kuwawezesha kina mama ili mchango wao utambulike na kuleta athari chanya katika jamii maana tunataka kila mwanamke anayejihusisha na mnyororo wa thamani katika uvuvi anakuwa na sehemu ya kutoa mawazo yake na kubadilishana uzoefu ili kwa pamoja wachangie uboreshaji wa uvuvi,” amesema Oliva.

Mratibu huyo amesema, “Jukwaa rasmi kitaifa lilifunguliwa 2017 ili kuwafikia wanawake wengi wakaanzisha Zone Chapters, Chapter ya Kanda ya Ziwa Victoria 2019, baadaye ikaja ya Uvuvi baharini, Kanda ya Ziwa Tanganyika na baadaye huko tutakuwa na linguine linalohusika na wavuvi kutoka katika maziwa madogo madogo.”

Awali, Mwenyekiti wa Taifa wa Mtandao wa Wanawake Wanaojihusisha na Shughuli za Uvuvi Tanzania (TAWFA), Beatrice Mmbaga amesema jukwaa hilo ni sehemu ya kutatua changamoto zinazowakabili kina mama walio katika sekta ya uvuvi.

“Nia ya kuanzisha chombo hiki ni kumfikia mama popote alipo anayejishusisha na samaki na mazao yake Tanzania nzima ndipo sasa tunashuka ngazi za chini katika Mikoa yetu, Kanda na Wilaya ili tuwe na sauti moja kwa sababu kina mama ndiyo asilimia kubwa wanajihusisha na samaki baada ya mavuvi hasa kwenye kuchakata na masoko lakini wana changamoto nyingi sana,” amefafanua Beatrice.

Kwa upande Mkurugenzi Msaidizi anayesimamia masuala ya Udhibiti Ubora na Mazao ya Uvuvi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Steven Lukanga amesema wanawake bado wanahitajika kupatiwa elimu ya uvuvi salama, na kukidhi mahitaji ya walaji.

“Kikubwa ni kuwajengea uwezo wanawake kutambua viwango vinavyopaswa kuzalisha yale mazao yanayowaendea walaji kwa kuzingatia viwango vilivyopo chini ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kwahiyo sisi kama wizara tunashirikiana nao kuhakikisha wachakataji wanawake wanakidhi viwango vinavyotakiwa,”amebainisha Lukinga.

Makamba afufua mradi uliokwama kwa miaka 24
Hakuna dalili za kumalizika vita Ukraine