Mtangazaji wa kituo cha runinga na redio cha Afrika Kusini, cha SABC amedai kuwa amepigwa kwa sababu za kiubaguzi wa rangi na vijana wa ‘kizungu’.

Samora Mangesi ametoa taarifa hiyo kwa umma kupitia mtandao wa Twitter akiweka picha zinazomuonesha alivyojeruhiwa vibaya.

Ameleza kuwa alikuwa anaendesha gari Ijumaa usiku akiwa na rafiki zake wa kike, ndipo walipoona gari lililopinduka na wakaamua kusimama kujaribu kutoa msaada. Lakini walipofika kwenye eneo la tukio, waliwakuta vijana wa kizungu ambao waliwaita ‘nyani’.

“Nilipoanza kuwahoji kwanini watuite sisi nyani, walinivamia na kunipiga hadi nilipopoteza fahamu,” Mangesi alieleza.

Anasema kuwa wakati wakiendelea kumpiga, mtu mmoja kati ya watesi wake alijaribu kumgonga na gari mmoja kati ya marafiki zake, tena wakati ambapo gari la wagonjwa (ambulance) lilikuwa limefika katika eneo la tukio na watu hao wakijaribu kukimbia.

Ameeleza kuwa baada ya tukio hilo, alijaribu kuachana na kilichotokea ili aendelee na maisha yake, lakini mwisho aliamua kuripoti polisi ili kutafuta haki yake na kwa faida ya wengi zaidi.

Msemaji wa polisi wa Afrika Kusini aliyefanya mahojiano na BBC amekiri kuwa tukio hilo limeripotiwa polisi na uchunguzi unaendelea.

Joshua Nassari avuliwa Ubunge
Mambo saba unayopaswa kuyajua baada ya ndege ya Ethiopia kuanguka

Comments

comments