Licha ya kuhusishwa sana na mipango ya usajili ndani ya Young Africans, uongozi wa Mtibwa Sugar umesema hauna mpango wa kumuacha kiungo wao mkabaji Abdul-halim Humud.

Msemaji wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema Humud bado ana mkataba na wakata miwa hao na hawafikirii kumruhusu akajiunge na Young Africans au timu nyingine yoyote hapa nchini.

“Humud ni mchezaji wetu muhimu, hatufikirii kumuacha akajiunge na timu yoyote hapa nchini labda apate nafasi nje ya nchi,” amesema Kifaru

“Tumemfanya Humud awe bora, ni mchezaji tunayemuhitaji sana katika malengo yetu ya msimu ujao hivyo ataendelea kubaki Manungu,” aliongeza Kifaru

Kifaru amesema Humud ni mfano wa kazi ambayo Mtibwa Sugar wamekuwa wakiifanya kwa miaka mingi kuimarisha viwango vya wachezaji pamoja na kuibua wachezaji wapya.

“Tunajivunia kuwa na rekodi ya kutoa wachezaji wengi ambao wanatamba hapa Tanzania. Mfumo wetu wa kukuza vipaji kuanzia U17 na U20 umekuwa na manufaa makubwa”

“Unaweza kusema Mtibwa Sugar ndio chuo kikuu cha kutengeneza vipaji vya wanasoka hapa nchini,” alitamba Kifaru

Mtibwa Sugar ndio mabingwa wa ligi ya soka ya vijana wakiwa na timu imara za U17 na U20.

Katika kikosi chao kinachoshiriki ligi kuu wanatumia wachezaji wengi wanaopita kwenye akademi yao.

Ruhsa kufanya mazoezi ya pamoja Italia
India yarudisha usafiri wa treni kwa tahadhari