Benchi la Ufundi la Mtibwa Sugar bado linaamini timu yao ina nafasi ya kupambana na kubaki Ligi Kuu kwa msimu ujao wa 2022/23, licha ya kupoteza mchezo dhidi ya KMC FC.

Mtibwa Sugar jana Alhamis (Mei 12) ilikua ugenini jijini Dar es salaam Uwanja wa Uhuru, ikicheza dhidi ya KMC FC iliyochomoza na ushindi wa mabao 3-2.

Kocha Msaidizi wa Mtibwa Sugar Awadh Juma amesema kupoteza mchezo huo haimaanishi timu yao imepoteza muelekeo wa kupambana, na badala yake wameyachukua matokeo hayo kama chachu ya kuongeza juhudi ili waweze kushinda michezo inayofuata.

Amesema Ligi Kuu msimu huu bado ina michezo kadhaa kabla ya kufikia kikomo chake, hivyo watapambana vilivyo ili kufanikisha lengo la kufanya vizuri na kubaki katika daraja hilo kwa msimu ujao.

“Ligi bado ipo wazi kwa sababu kila timu ina uwezo wa kushinda na kwenda juu katika msimamo, Mtibwa Sugar ni miongoni mwa timu ambazo zina hiyo nafasi, kwa hiyo hatujakata tamaa, tunaendelea kupambana na tutafikia lengo letu,”

“Ukiiweka Mtibwa Sugar katika kundi la timu ambazo zitashuka daraja msimu huu, kwangu mimi ninakataa hilo kwa sababu timu yangu ipo vizuri, ninaamini inaweza kufanya vizuri zaidi ya hapa, haimaanishi kupoteza dhidi ya KMC FC ndio iwe sababu za kuishusha timu yetu.”

“Kabla ya kuanza kwa mchezo wa jana nilisema KMC FC ni timu nzuri, ina uwezo wa kupata ushindi ugenini na nyumbani, wameweza kupata ushindi wakiwa nyumbani kwahiyo moja ya matarajio ya matokeo nilioyategemea yametokea, lakini nasisitiza Mtibwa Sugar bado tupo vizuri.”

Katika hatua nyingine Awadh Juma amesema wameanza maandalizi ya mchezo ujao dhidi ya Coastal Union ambao utaunguruma juma lijalo katika Uwanja wa Mtibwa Complex- Manungu.

“Tumeshaanza maandalizi ya kuelekea mchezo wetu ujao dhidi ya Caostal Union, tunaaini tukiwa nyumbani tutafanya vyema kwenye mchezo huo,”

“Lengo letu ni kurudi katika njia ya ushindi kupitia mchezo huu, hivyo niwatoe wasiwasi mashabiki wa Mtibwa Sugar kwa kusema tutapambana na kupata alama tatu nyumbani.” amesema Awadhi Juma

Muchachu aitahadharisha Young Africans
Ushindi dhidi ya Mtibwa, Kocha KMC FC aitaja Real Madrid