Alipita Salum Mayanga akaondoka akamwachia Mecky Mexime ambaye baada ya kuondoka kwake akamwacha Zuber Katwila, sasa hivi Katwila kaondoka amemwacha Vicent Barnabas halafu Awadh Juma kachukua nafasi ya Barnabas kwenye timu ya vijana.

Wote hao ni wachezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar kabla ya kuingia kwenye ukocha, na bahati nzuri wamepata nafasi na kuaminiwa kuanza kufundisha sehemu ambayo walicheza.

Mtibwa ina mfumo mzuri wa kuanza kuwaendeleza wachezaji kuanzia timu ya vijana halafu inawapa nafasi kwenye timu ya wakubwa na baadaye kwenye ukocha.

Miaka ya mbele hatutashangaa tumwona mchezaji kama Dickson Job anakuwa sehemu ya benchi la ufundi la Mtibwa. Ameanzia timu ya vijana, akaingia timu ya wakubwa halafu kwenye ukocha, ni kama ilivyokuwa kwa Pep Guardiola na Barcelona.

Mtibwa inafanya kitu kizuri na inatoa fundisho kwa vilabu vingine kuwa na malengo na wachezaji hata baada ya kustaafu kucheza.

Kwa mfano wakati Yanga inaacha wachezaji wake kabla ya kuanza msimu huu, sikutegemea kumuona Mrisho Ngasa akiondoka kwa namna ile.

Ilikosekana nafasi yoyote kwa mchezaji kama Ngasa kwa namna alivyoitumikia Yanga kwa mapenzi ya dhati kwa sababu Ngasa hajawahi kuficha mapenzi yake kwa Yanga.

Nilitarajia kumuona Ngasa akipewa majukumu mengine na kuendelea kubaki kwenye timu kama ambavyo iliwahi kuwa kwa Nsajigwa na Cannavaro.

Pacha waliotenganishwa warejea nyumbani
Sudan kuondolewa katika orodha ya kufadhili magaidi