Mkuu wa Idara ya Habari ya Klabu ya Mtibwa Sugar Thobias Kifaru ameitahadharisha Azam FC kuelekea mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ utakaozikutanisha timu hizo kati ya Machi 30 hadi Aprili 2.

Miamba hiyo ilipangwa kukutana katika hatua hiyo, baada ya kupangwa kwa Droo ya Robo Fainali ya ASFC chini ya usimamizi wa Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’ na Wadhamini Wakuu Azam Media.

Kifaru amesema Mtibwa Sugar imekuwa na malengo makubwa katika michuano ya ASFC msimu huu 2022/23, hivyo Azam FC inapaswa kujipanga kabla ya hawajakutana kwenye mchezo huo ambao utapigwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam.

Amesema wanausubiri mchezo huo kwa hamu kubwa, huku Kocha Mkuu Shaban Mayanga akiendelea kukisuka kikosi chake, katika kipindi hiki ambacho Ligi Kuu imesimama kupisha Kalenda ya FIFA.

“Tunaisubiri kwa hamu mchezo huo, Mtibwa Sugar tuna malengo ya kucheza nusu fainali hatutaki tena kushiriki michuano hii bali tunahitaji kushindana ili kufikia malengo.”

“Azam FC tunawahamu vizuri, wana kila kitu, ubora, wachezaji lakini kwa hili hatuwezi kuruhusu watuharibie malengo Lazima jasho limwagike uwanjani.” Amesema Kifaru

Michezo mingine ya Robo Fainali ASFC, Mabingwa watetezi Young Africans watakuwa wenyeji wa Geita Gold FC, huku Simba SC ikipewa Ihefu FC na Singida Big Stars itapapatuana na Mbeya City.

Kocha US Monastir aitega Young Africans
Kaze afichua mbinu za kuisambaza US Monastir