Aliyekuwa Mbunge wa Temeke kwa tiketi ya Chama Cha Wananchi (CUF), Abdallah Mtolea amejiunga rasmi na Chama Cha Mapinduzi (CCM), saa chache baada ya kutangaza kujiuzulu Ubunge leo mchana.

Mtolea ambaye alitangaza rasmi kujiuzulu alipopewa nafasi ya kuchangia bungeni, ametangaza kujiunga na CCM leo usiku mbele ya Katibu Mkuu wa chama hicho tawala, Dkt. Bashiru Ally.

Awali, akitangaza uamuzi wake wa kujiuzulu ubunge, Mtolea alivialika vyama vyote vya siasa nchini amabavyo vinaamini anaweza kufanya navyo kazi isipokuwa CUF, kumpa nafasi hiyo.

Tofauti na wabunge wengi wa upinzani waliojiuzulu nafasi hiyo na kujiunga na CCM, Mtolea alifafanua kuwa kilichomfanya kujiuzulu ni mgogoro wa kambi mbili zilizo ndani ya chama chake ambao umefikia hatua ya kutishiana maisha.

Alisema kuwa upande wa wale ambao wanamuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba kama Mwenyekiti wa CUF walimtishia na kwamba kulikuwa na mpango wa kumvua Ubunge ndani ya wiki mbili zijazo.

Alitoa shukurani zake kwa Spika wa Bunge, viongozi wa Serikali ndani ya Bunge pamoja na Kambi rasmi ya upinzani kwa kushirikiana naye kufanya kazi.

Mtolea pia alimshukuru Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwa kumuamini lakini alisisitiza hana budi kuondoka kwani mgogoro huo unamfanya kushindwa kutekeleza ipasavyo majukumu yake kama Mbunge.

Spika Ndugai afananisha ya Mtolea na Lowassa
Hatua kali kuchukuliwa dhidi ya watakaoingiza bidhaa za magendo nchini

Comments

comments