Mtoto wa kiume wa Bobby Brown na Kim Ward mwenye umri wa miaka 28, Bobby Brown Jr. amekutwa akiwa amefariki dunia nyumbani kwake jijini Los Angeles, Jumatano wiki hii.

TMZ imeripoti kuwa, Mamlaka za Los Angeles zinaendelea kufanya uchunguzi wa kifo cha kijana huyo wa mwanamuziki nguli na mkongwe nchini Marekani.

Kijana huyo alionekana zaidi alipokuwa na umri wa miaka 13 kwenye ‘reality show’ ya familia iliyojulikana kama ‘Being Bobby Brown’.

Hili ni pigo la tatu kwenye familia ya Bobby Brown kwa njia inayofanana. Ikumbukwe kuwa Julai 26, 2015, mtoto wa kike wa Bobby Brown, Bobbi Kristina alikutwa akiwa hajitambui bafuni, nyumbani kwake Georgia, Marekani. Kristina alikuwa mtoto wa Bobby Brown na mwanamuziki Whitney Houston.

Kristina alikimbizwa hospitali akiwa hajitambui na alikaa kwenye mashine ya kumsaidia kupumua kwa miezi kadhaa kabla ya kufariki dunia. Mamlaka zilieleza kuwa kifo chake kilitokana na kuzama ndani ya bafu (kwenye ‘bathtub), na uchunguzi wa mwili wake ulibaini kuwa alikuwa amekunywa pombe na madawa ya kulevya aina ya cocaine.

Kifo cha Kristina kilifanana na cha mama yake, Whitney Houston ambaye alifariki dunia miaka mitatu kabla katika Hotel ya Beverly Hilton.

Bobbi Kristina alizikwa pembeni ya mama yake, Whitney Houston katika eneo la Fairview Cemetery, Westfield, New Jersey.

Bobby Brown na Houston walikuwa wana ndoa kati ya mwaka 1992 hadi 2007. Hata hivyo, Bobby Brown alikuwa na uhusiano na Kim Ward kwa kipindi cha miaka 11, uhusiano uliokuwa unazima na kuwaka mara kwa mara hadi alipofunga rasmi ndoa na Houston.

Mtoto wa miaka 9 anusurika kuchinjwa na baba yake
Simba yawasili Arusha, Morrison ndani