Mtoto mwenye umri wa miaka 9, mkazi wa Kitongoji cha Batini, Wilayani Gairo, Mkoani Morogoro, amenusurika kifo baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali maeneo ya shingoni na baba yake mzazi aliyefahamika kwa jina la Yakobo Taolo (38), huku chanzo kikidaiwa kuwa ni imani za kishirikina.

Kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro SACP Wilbroad Mutafungwa, amesema kuwa tukio hilo limetokea Novemba 15 mwaka huu, majira ya 7:00 usiku ambapo baba wa mtoto huyo alivamia chumba alicholala binti yake huyo, anayesoma darasa la pili katika shule ya msingi Kibedya na kuanza kumshambulia kwa sime.

Kamanda Mutafungwa ameongeza kuwa mara baada ya baba huyo kutekeleza tendo hilo la kutaka kuua, alitokomea pasipojulikana kabla ya jeshi la polisi kumkamata akiwa nyumbani kwa Robart Chidaka (45), mkazi wa Kibedya ambaye anashikiliwa na jeshi hilo.

Kamanda Mtafungwa amesema kuwa baada ya baba huyo kushikiliwa na jeshi la polisi, alianza kuumwa na kukimbizwa katika kituo cha afya Gairo kwa ajili ya matibabu na baadaye aligundulika kuwa na tatizo la kupumua na ilipofika alfajiri ya Novemba 16 mtuhumiwa huyo alipoteza maisha.

Mtoto huyo aliyenusurika kuuawa kwa sasa anapatiwa matibabu katika kituo cha afya Gairo.

BOT yachukua usimamizi China Commercial Bank
Mtoto mwingine wa Bobby Brown akutwa amefariki nyumbani kwake