Wakati Uingereza leo ikijiandaa kusherehekea ndoa ya kifalme kati ya Prince Harry na aliyekuwa muigizaji wa Marekani, Meghan Markle, nchini Uganda kutakuwa na tukio la aina yake la kuhuisha ndoa kati ya mtoto wa kwanza wa Rais wa Afrika Kusini aitwaye Andile Ramaphosa na mpwa wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Amama Mbabazi.

Mbabazi aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Uganda kwa kipindi cha miaka tisa na baadaye kuwa mmoja kati ya wapinzani wakuu wa Serikali, akigombea urais dhidi ya Rais Yoweri Museveni akichuana pia na Dkt. Kizza Besigye, katika uchaguzi wa mwaka 2016.

Andile, mtoto wa Rais Cyril Ramaphosa ameingia jana mchana nchini Uganda akiwa na msafara wake kwa lengo la kumuoa Bridget Birungi Rwakairu ambaye alikuwa mpenzi wake wa siku nyingi, kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor.

Kijana huyo ameongozana na mama yake, wajomba zake pamoja na shangazi zake.

Sherehe ya kitamaduni inayofahamika kwa jina la ‘Okhushaba’, ikiwa na maana ya ‘kuomba’ itafanyika katika makazi binafsi ya Amama yaliyoko jijini Kampala.

Katika sherehe hizo, familia za pande mbili za wachumba wanaotarajia kufunga ndoa hutambulishwa rasmi na baadaye kufanya makubaliano ya mahari inayolipwa na familia ya bwana harusi mtarajiwa.

“Kwa mujibu wa mila na desturi zetu, sherehe ya ‘Okhusaba’ itafanyika Mei 19, katika eneo la Nyanyi Gardens ambalo ni eneo la Mheshimiwa Amama Mbabazi,” inaeleza taarifa iliyotolewa na familia ya Amama.

Andile mwenye umri wa miaka 36, ambaye ni kijana wa rais Ramaphosa, ni mtaalam wa masoko na biashara, hivi sasa anafanya kazi kama Mtendaji Mkuu wa Timu ya Mikakati katika Benki ya Afrika Kusini ya Macquire.

Mchumba wake huyo ambaye wamekuwa katika uhusiano kwa kipindi cha miaka 10, ana umri wa miaka 37. Wawili hao wana mtoto mwenye umri wa miezi miwili.

Video: Makonda ayakana Makontena Bandarini, CCM inajiua
Makonda kuwashughulikia watoto wa mitaani