Hatimaye leo mmiliki wa mtandao wa Facebook, Mark Zuckerberg ametunukiwa shahada ya heshima ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Harvard, baada ya miaka 12 tangu alipoamua kuacha masomo yake chuoni hapo na kujikita katika kukuza mtandao wake.

Zuckerberg alipewa nafasi ya kutoa nasaha na busara zake kwa wahitimu wa mwaka huu, waliotunukiwa shahada na chuo hicho chenye heshima kubwa duniani.

Katika hotuba yake, aliwaasa wanafunzi hao kuhakikisha wanajikita katika kufanikisha ndoto zao kubwa kwa kuwaleta pamoja watu wengi zaidi kwa faida ya jamii nzima. Aliongeza kuwa teknolojia nyingi ikiwa ni pamoja na zilizotokana na Facebook, zimeleta mabadiliko duniani ingawa zina changamoto zake.

“Tumetembea umbali huu chini ya muongo mzima, tukisoma mawazo yanayofanana na kupitia mafunzo yaleyae. Tumepita njia tofauti kufika hapa, lakini leo nataka kushiriki nanyi nilichojifunza kuhusu kizazi chetu na dunia tunayoijenga pamoja,” alisema bilionea huyo kijana.

Aliwahamasisha wanafunzi hao kuhakikisha wanawajibika kuleta mabadiliko makubwa kwa kizazi hiki sio tu kwa kutengeneza ajira bali pia kutengeneza ‘nia’.

Kwa mujibu wa Facebook, Zuckerberg amekuwa mtu mwenye umri mdogo zaidi (33) kuwahi kupewa nafasi ya kutoa hotuba yake katika sherehe za chuo kikuu hicho.

Video: Watu 4 waliopasua maiti kutoa dawa za kulevya wakamatwa
Serikali yaahidi kuinua soka la vijana nchini