Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe amejitokeza hadharani kwa mara ya kwanza tangu jeshi la nchi hiyo liliposhika nchi kwa madai ya kuwasaka wahalifu wanaomzunguka.

Mugabe ameonekana leo akisindikizwa na maafisa wa jeshi ambapo alihudhuria mahafali ya Chuo Kikuu Huria cha Zimbabwe jijini Harare akiwa ndiye Mkuu wa chuo hicho. Alipolewa kwa shangwe kubwa na wananchi waliokuwa kwenye mahafali hayo.

Hata hivyo, mkewe Grace na Waziri wa Elimu, Jonathan Moyo ambao wamekuwa wakiongozana naye kwenye matukio mengi hawakuonekana leo.

Taarifa zinadai kuwa wawili hao walikuwa chini ya usimamizi wa kijeshi kutokana na mgogoro wa madaraka unaoendelea katika chama cha Zanu-PF.

Inaelezwa kuwa baada ya kumfuta kazi Makamu wa Rais ya nchi hiyo, Emmerson Mnangagwa, Mama Grace alikuwa na nafasi kubwa ya kumrithi Mugabe.

Tamko la awali la jeshi lilieleza kuwa hawatasita kuingilia kati mgogoro wa madaraka na kuona waliopigania uhuru wa nchi hiyo wakifukuzwa.

Jeshi la nchi hiyo limeeleza kuwa limefanya mazungumzo na Mugabe na kwamba litautangazia umma walichokubaliana hivi karibuni.

Aidha, mpinzani wake mkuu wa muda mrefu, Morgan Tsvangirai amemtaka Rais Mugabe kujiuzulu huku akiitisha maandamano siku ya Jumamosi.

Kaburu, Aveva warejeshwa rumande hadi Novemba 30
BoT yakanusha Amana Bank kufungwa