Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe ameripotiwa kumpiga marufuku mtumbuizaji wa kike wa Afrika Kusini, Zodwa Wabantu kutumbuiza nchini humo kutokana na tabia yake ya kupanda jukwani bila kuvaa nguo za ndani.

Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kufungua kituo cha taarifa za jamii cha Bindura nchini humo (Bindura Community Information Centre) hivi karibuni, Rais Mugabe alisema kuwa amemzuia Zonda kwakuwa vitendo vyake vya kupanda jukwaani bila nguo ya ndani haviendani na maadili ya nchi hiyo.

Mugabe aliwaomba radhi wanaume ambao alidai kuwa amesikia wakilalamika kuhusu uamuzi huo.

“Hatutaki mtu yeyote msumbufu kuja nchini kwetu akiwa mtupu kwa ajili ya kusababisha matatizo. Nini hasa lengo lake la kuja hapa? Rais  Mugabe alihoji.

“Ili wanaume waweze kukuona? Poleni. Tumewaangusha wanaume wengi ambao walikuwa wanalalamika. Nimesikia walikuwa wanataka [Zodwa] aje. Hayo ni mawazo ambayo hatuyataki, acha hayo yafanyike huko anakotoka (Afrika Kusini),” anakaririwa na mtandao wa Zimbabwe wa Bulawayo24.

Zodwa Wabantu

Zodwa ambaye ni mtumbuizaji maarufu anayepanda jukwaani akiwa na nguo zake isipokuwa nguo za ndani, alikuwa amealikwa kushiriki tamasha maarufu la kimataifa jijini Harare la ‘Harare International Carnival’.

Vyombo vya habari vya Zimbabwe vimeeleza kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Maadili ambaye pia ni Waziri wa zamani wa nchi hiyo, Aeneas Chigwedere alisema kuwa vitendo vya Zodwa ni kinyume cha maadili na kwamba uamuzi wa Serikali umelenga kuwalinda vijana na jamii kwa ujumla dhidi ya kumomonyoka kwa maadili.

Tamko la Serikali hiyo lilitolewa muda mfupi baada ya baadhi ya wasanii wa nchi hiyo kulalamikia kitendo cha waandaaji wa tamasha hilo kutaka kuwatumia zaidi wasanii wa nje ya nchi na kuwaacha wasanii wa ndani.

Video: Jambazi aliyeongoza mauaji ya Polisi 8 Kibiti auawa
Bunge laziunganisha TRL na RAHCO