Mkurugenzi Mtendaji wa Zanzibar Media Corporation, Muhammed Seif Khatib amefariki dunia leo asubuhi Februari 15, 2021.

Uongozi wa Zanzibar Media Corporation pamoja na Mkurugenzi wa Maelezo Zanzibar wamethibitisha kutokea kwa kifo hicho na kueleza kuwa taratibu za mazishi zitatolewa na familia yake hii leo.

Khatib ni mwanasiasa aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Uzini, Unguja na amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya CCM na nafasi kadhaa uwaziri kama vile Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Alikuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) tangu mwaka 1978 hadi 1983 na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kuanzia mwaka 1978 hadi 2002.

Aidha atakumbukwa kwa utaalamu wake wa lugha ya Kiswahili ambapo hadi anafariki dunia alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA).

Hadi umauti unamkuta alikuwa akimiliki vyombo vya habari vya Zenji FM/Zenji TV pamoja na gazeti la Nipe Habari.

Kim Paulsen kocha mpya Taifa Stars
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 15, 2021