Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imekanusha taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mwanamke mmoja mgonjwa anayedaiwa kujigeuza ndege usiku na kurudi kuwa binadamu asubuhi, aliyekamatwa na wagonjwa wenzake.

Taarifa hiyo ya Hospitali ya Muhimbili imesema kuwa imejiridhisha na uchunguzi uliofanyika na wamebaini kuwa picha na video hiyo hazihusiani na Hospitali ya Muhimbili kimazingira na katika takwimu zao hawana mgonjwa kama huyo.

“Kwanza hatuna mgonjwa huyo, pili, hatuna wodi zinazofanana na hiyo katika hospitali zetu (Upanga na Mloganzila), tatu, wauguzi wanaoonekana katika video hiyo hawajavaa sare za hospitali zetu,” imesema taarifa hiyo.

“Tunawaomba wananchi na watumiaji wa huduma katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (Upanga na Mloganzila) kutokuwa na hofu juu ya taarifa hizo kwani siyo za kweli“, imeongeza taarifa hiyo.

Hata hivyo, kupitia taarifa hiyo, uongozi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili umesema kuwa unafanyia kazi chanzo cha taarifa hiyo kwa kushirikiana na mamlaka husika ikiwemo vyombo vya usalama.

Video inayosambaa mitandaoni inamuonesha mwanamke huyo akiwa amezungukwa na wagonjwa, waangalizi wa wagonjwa na wauguzi kwenye Wodi ya hospitali akikemewa na kutakiwa aondoke baada ya kukutwa na sintofahamu hiyo ya kujigeuza kutoka kuwa ndege hadi kuwa binadamu.

Wenye magari yaliyofungwa ving'ora watakiwa kuving'oa
Mo Dewji kugharamia awamu ya kwanza ujenzi wa uwanja wa Simba