Tanzania imezihakikishia Kampuni za Kifaransa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni salama na kuwasihi kuwekeza kwa wingi hapa nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kongamano lilowakutanisha Mawaziri wa Kisekta, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa Jijini Dar es Salaam.

Balozi Mulamula, amesema Serikali imewahakikishia wafanyabishara na wawekezaji wa kampuni za Kifaransa kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inajenga na inaendelea kuboresha mazingira rafiki ya uwekezaji kwa kuondoa kero mbalimbali zilizokuwa zinawakabili wawekezaji hapa nchini.

Ameongeza kuwa Wafaransa wamekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania kwa muda mrefu na hivi sasa wamekuwa na shauku ya kufanya biashara na kuwekeza kwa wingi hapa nchini

Takwimu zinaonesha watalii kutoka Ufaransa kuja Tanzania kila mwezi ni zaidi ya watalii 7000 wanaokuja kutembelea vivutio mbalimbali hapa nchini, hivyo ni changamoto kwetu kuchangamkia fursa hii adhimu.

Kwa upande wake, Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Franck Riester amesema Ufaransa inatambua jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji mambo ambayo pia yanatiliwa mkazo na serikali ya Ufaransa.

“Ufaransa imedhamiria kuongeza ushirikiano na Tanzania na kama mlivyoshuhudia leo tumeanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Paris hadi Zanzibar ambao ulisimama tangu mwaka 1974, huu ni mwanzo mzuri” Amesema Riester.  

Riester amesema kuwa wataendelea kuwaeleza na kuwahamasisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Ufaransa juu ya fursa mbalimbali zinazopatika Tanzania ikiwemo katika sekta ya Nishati, Utalii, Viwanda, Usafirishaji pamoja na Uwekezaji ili kuja kuwekeza na kukuza ucbumi wa pande zote mbili.

Mawaziri wa Kisekta waliohudhuria kongamano hilo ni Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro, Waziri wa Nishati, January Makamba Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Prof. Makame Mbarawa (Mb) Waziri wa Uwekezaji – Zanzibar Mhe. Mudrick Soraga, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb) na Waziri wa Ofisi ya Rais Uwekezaji Mhe. Geoffrey Mwambe.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongea na washiriki wa Kongamano lililowakutanisha Mawaziri wa Kisekta, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji wa Ufaransa, Mhe. Franck Riester akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kumalizika kwa Kongamano lililowakutanisha Mawaziri wa Kisekta, wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Ufaransa Jijini Dar es Salaam
Magori awatoa hofu Jwaneng Galaxy
Wachezaji wamfariji Paul Godfrey Boxer