Kamanda wa Polisi mkoa wa kipolisi Kinondoni, Edward Bukombe ametoa taarifa kuwa Mume wa Marehemu Mercy Mkandara, Erick Samson amekiri mwenyewe kumuua mkewe kwa kutumia kifaa kizito (spana ya bomba) kwa kumpiga kichwani.

Kamanda Bukombe amesema mtuhumiwa Samson amefikia hatua hiyo baada ya kuwekwa chini ya ulinzi na kuhojiwa na jeshi la polisi baada ya ripoti ya daktari kutilia shaka chanzo cha kifo cha Mercy kuwa sio kujigonga kama mume wake alivyoeleza awali.

“Madaktari walivyofanya utafiti wao wakathibitisha kama hilo ni jeraha ambalo limeshababishwa na mtu mwingine, kwahiyo baada ya mahojiano ya kina huyo mwanaume baadaye aliweza kukiri mwenyewe kwa kinywa chake kwamba ni kweli alihusika katika mauaji hayo,” ameeleza Kamanda Bukombe.

Amesema kuwa aliwapeleka polisi nyumbani kwake ambapo alificha kifaa alichotumia kumpiga kwenye utosi marehemu na kupelekea kifo chake, ambacho alikificha jikoni kwenye paa la nyumba.

Aidha, amesisitiza kuwa kwakuwa mtuhumiwa amekiri mwenyewe kwa kinywa chake, hatua nyingine za kisheria zitakapo kamilika atapelekwa Mahakamani.

Mercy alifariki dunia usiku wa kuamkia Juni 16, 2020, huku Mumewe akieleza kuwa kifo chake kimetokana na shoti ya umeme na kujigonga ambapo majiriani zake na ndugu walianza kutilia shaka sababu hiyo kwani alikutwa na majeraha makubwa kichwani.

Mbaroni kwa kumtorosha na kumfanyia shambulio la aibu mtoto wa miaka 14
TPLB kuijadili Azam FC