Waziri wa zamani wa Elimu na Utamaduni, Joseph Mungai amekana kuwa chanzo cha kuporomoka kwa elimu nchini na kusukuma mzigo wa lawama zote kwa utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne iliyoongozwa na Dk. Jakaya Kikwete.

Mungai ambaye alikuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni katika Serikali ya Awamu ya Tatu na kufanya mabadiliko mengi ambayo baadhi ya watu wanadai yalichangia kuporomoka kwa elimu, amesema kuwa alifanya kazi kubwa ya kuboresha elimu lakini ilianza kubomolewa mwanzoni mwa awamu iliyofuata.

“Nilijisikia vibaya kuona kazi nzuri tuliyoifanya chini ya uongozi wa Rais Benjamin Mkapa (Awamu ya Tatu) inabomolewa katika mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Nne,” Mungai aliiambia Mwananchi.

Aliongeza kuwa alisononeka kuona hali hiyo lakini pia kutosikilizwa katika kile alichoshauri. Msomi huyo ambaye alistaafu siasa amesema kuwa aliwatahadharisha waliokuwa madarakani kuwa elimu ingeanza kuporomoka kutokana na uamuzi wao, matokeo yaliyoanza kuonekana miaka michache baadae.

“Baada ya mwaka 2007, matokeo ya mitihani ya darasa la saba na kidato cha nne yalianza kushuka mwaka hadi mwaka,” alisema Mungai. ”Mwaka 2012 idadi ya waliofeli ilifika asimia 60.”

Alisema kutokana nahali hiyo hadi sasa hata vyuo vikuu vinapokea wanafunzi ambao hawajui vizuri kiingereza kwakuwa mfumo wa kuwa na masomo ya kiingezeza kwa wanafunzi wote wa kidato cha tano na sita kwa ajili ya kuwaandaa na elimu ya chuo kikuu ulifutwa.

Katika hatua nyingine, Mungai alikana kufuta michezo mashuleni na kueleza kuwa alichoagiza ni michezo ifanyike baada ya muda wa masomo pamoja na kufuta michango ya mashindano ya michezo mashuleni.

Akizungumzia anachojivunia alipokuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni, Mungai alisema kuwa anajivunia kufuta ada na kuifanya elimu ya msingi kuwa ya bila malipo na ya lazima kwa kila mtoto wa kuanzia miaka saba hadi 13.

Pia, alisema kuwa wanajivunia kuanzisha masomo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika vyuo vya ualimu na mtaala mpya katika shule za sekondari.

GK aitamani Bifu ya Diamond na Ali Kiba, ’ningeichochea’
Paul Pogba Aomba Muda Zaidi