Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kwamba hatamuunga mkono mgombea yoyote hata kwenye uchaguzi mkuu wa Kenya Agosti 9, 2022.

Akizungumza siku ya,Jumatatu Januari 24 kwenye mahojiano na runinga ya New Vision, Museveni alitoa bayana msimamo wa serikali yake ya iwapo angemuunga mkono Naibu Rais ikizingatiwa wamekuwa na uhusiano wa karibu kwa miaka kadhaa.

Hata hivyo, Museveni alisema nchi yake itazingatia sera za kutoingililia uchaguzi wa mataifa ya nje, akidokeza kuwa Uganda imewahi kutaabika kufuatia kuingililiwa na mataifa mengine.

“Uchaguzi wa Kenya au nchi nyingine ni suala linalowahusu raia wa taifa hilo. Raia hao ndio watakaoamua wanachopaswa kufanya. Kumuunga Ruto, siwezi kufanya maaamuzi kama hayo. Hatutawahi kupendelea upande wowote,” Rais huyo alibainisha.

Wakati wa chaguzi kuu ya miaka ya 2016 na 2021, Ruto alimfanyia kampeni za urais Museveni na chama chake cha National Resistance Movement (NRM).

Katika hatua nyingine, Waziri wa Uchukuzi James Macharia amefichua mipango ya kumfanyia kampeni waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, ili aibuke mshindi kwenye uchaguzi wa urais mwaka huu.

Akizungumza wakati wa mkutano na viongozi wa mashinani Jumatatu Januari 24, katika Kaunti ya Murang’a, Macharia alidokeza kuwa wataanza kampeni za miezi sita ili kumpigia debe kinara wa ODM.

Alifafanua kuwa Raila anatosha kuwa rais ikizingatiwa kuwa ana tajriba katika siasa na hana shaka ataendeleza ajenda za maendeleo za Rais Uhuru Kenyatta huku akitetea wazi uamuzi wake wa kuunga mkono mgombea wa urais wa Azimio la Umoja, akidokeza kwamba yeye ni mwananchi wa kawaida ambaye anaelewa vyema masuala tata yanayowakumba Wakenya.

Wakati wa mkutano huo, waziri huyo alimtaja Raila kuwa rais wa tano na kuongeza kwamba waziri mkuu huyo wa zamani, ndiye atakayeibuka mshindi kwenye uchaguzi mkuu wa urais wa Agosti 9, ikilinganishwa na Naibu Rais William Ruto.

Macharia alifafanua kuwa kikosi cha kampeni kitahakikisha kuwa asilimia 98 ya waliojitokeza kupiga kura kwenye uchaguzi wa 2017, itajitokeza vivyo hivyo kumpigia kura Raila.

Watuhumiwa wa mauaji ya mwanamke gesti wakamatwa
Ahmed Ally: Gape la Point 10 halitutishi