Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amezungumzia kwa mara ya kwanza hali ya mwanamuziki, Bobi Wine ambaye pia ni mbunge nchini humo, kufuatia taarifa kuwa alipigwa na kikosi maalum cha ulinzi wa rais kiasi cha kushindwa kutembea au kuzungumza.

Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotoka jana, Museveni amewahakikishia wananchi wa Uganda kuwa hali ya kiafya ya Bobi Wine ni nzuri na kwamba kilichoelezwa na vyombo vya habari ni uzushi uliokithiri.

Bobi Wine anashikiliwa na jeshi la nchi hiyo kwa tuhuma za kufanya uhaini na kukutwa na silaha za moto kinyume cha sheria.

“Habari. Siku kadhaa zimepita wakati kile ambacho Rais [Donald] Trump alikiita wazalishaji wa ‘habari feki’, hususan gazeti la Monitor na Televisheni yao, NTV wakieleza kuwa mjukuu wetu, asiye na nidhamu Bobi Wine yuko kwenye hali mbaya, hawezi kungumza n.k,” ameeleza.

“Wameendelea kuripoti kuwa wakati wa kuwakamata wabunge, vyombo vya usalama viliweza kumuumiza vibaya Bobi Wine. Nimeamua kuwasiliana na madaktari wa jeshi kwa sababu, kutokana na jeshi letu kuwa na nidhamu, madaktari wa jeshi wamekuwa wakichukua tahadhari katika hali kama hiyo.

“Bobi Wine ameangaliwa na madaktari wa Arua, Gulu na Kampala. Hana majeraha ya kifua au kichwa au kuvunjika mfupa, wameniambia hilo,” aliandika Rais Museveni.

Baada ya kutolea ufafanuzi suala hilo ambalo limezua gumzo na kusababisha Marekani kuonya kuhusu hali ya vurugu dhidi ya wanasiasa nchini humo, Museveni aliendelea kukemea vitendo vya vurugu vinavyofanywa na baadhi ya wafuasi wa vyama vya upinzani.

“Nataka kuwataarifu kuwa Kitendo cha mataifa ya nje kutaka kuingilia demokrasia yetu hakikubaliki. Hatutavumilia vitisho vya aina yoyote iwe ni kwa maneno au kwa vitendo. Inatosha sasa. Vyombo vya habari pia vinaonywa. Fanyeni jukumu lenu, wekeni mizania sawa kwenye habari zenu,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo ya Rais Museveni.

Taarifa za awali zilidai kuwa mwanasheria wa Bobi Wine aliyehudhuria kesi ya uhaini dhidi ya mteja wake kwenye mahakama ya kijeshi, alisema kuwa mbunge huyo alikuwa ameumizwa vibaya na kwamba hakuwa anaweza kuongea wala kutembea. Ilielezwa kuwa alipelekwa mahakamani hapo akiwa amebebwa.

Video: Drake amrushia kombora Kanye West jukwaani
Ndugulile apiga marufuku watu kujipima Ukimwi