Kiungo na nahodha wa timu ya taifa ya Ivory Coast, Gnégnéri Yaya Touré, ameutaka uongozi wa klabu ya Man city, kumuweka wazi juu ya suala la kuendelea kubaki klabuni hapo ama kuachana nae itakapofika mwishoni mwa msimu huu.

Toure amewasilisha suala hilo katika bodi ya viongozi wa Man city, kupitia kwa wakala wake anayetokea nchini Urusi, Dimitry Seluk kufuatia tetesi zinazoendelea kutawala katika vyombo mbalimbali vya habari kila kukicha.

Taarifa zilizopo zinadai kwamba, kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32, hayupo katika mipango ya meneja mpya wa Man City, Pep Guardiola ambaye ataelekea Etihad Stadium mwishoni mwa msimu huu, kuchukua pahala pa Manuel Pelegrini.

Seluk, amesema juma lililopita alikua na kikao na viongozi wa klabu ya Man City ili kujua ukweli wa jambo hilo, lakini mpaka sasa hakuna muafaka wowote ambao umeshapatikana zaidi ya kuendelea kutolewa kwa tetesi.

Amesema ni bora viongozi wa Man City wakawa wazi katika jambo hilo, ili yeye na mchezaji wake wafahamu hatma yao huko Etihad Stadium, na kujipanga kusaka mahala pengine pa kumuwezesha Toure kucheza soka lake kwa utulivu na Amani.

Toure kwa sasa anapokea mshahara wa paund laki mbili na ishiriki elfu (220,000) kwa juma, hali ambayo inachangia kukaa kimya kwa viongozi wa Man City kwa kuhofia endapo watavunja mkataba, itawagharimu kiasi kikubwa cha pesa ambacho kitalipwa kwa kiungo huyo.

Katika hatua nyingine Seluk amepasua ukweli wa mambo ambao umekua ukijifichwa kwa muda mrefu kuhusu suala la kuondoka kwa Toure, ambapo amedai kwamba mashabiki wamekua na muono tofauti na meneja mpya Pep Guardiola, kwa kutaka kumuona kiungo huyo akiendelea kubaki klabuni hapo, kutokana na kuipenda huduma yake ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio yaliyopatikana tangu aliposajiliwa mwaka 2010.

Pep Guardiola amekua hana mahusiano mazuri na Yaya Toure, tangu aliporidhia kumuondoa kwenye kikosi cha Barcelona mwaka 2010 na kumuuza kwenye klabu ya Man City.

Mpaka sasa Toure ameshaitumikia Man City katika michezo 188 na kufanikiwa kufunga mabao 54, huku akichangia kwa kiasi kikubwa pasi za magoli yaliyofungwa na washambuliaji wa klabu hiyo.

Liverpool Wasubiri Droo Ya Robo Fainali Europa League
Roy Hodgson Amuita Kikosini Danny Drinkwater