Mchezao uliokua unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wengi dunaini, kati ya timu ya taifa ya Brazil dhidi ya timu ya taifa ya Argentina ambao ulipangwa kuchezwa usiku wa kuamkia hii leo, uliahirishwa saa moja kabla ya kipyenga hakijapulizwa.

Mchezo huo ambao siku zote umekua na mvuto wa aina yake kutokana na upinzani uliokithiri baina ya mataifa hayo mawili kwenye soka, uliahirishwa kutokana na mvua kubwa kunyesha mjini Buenos Aires na kusababisha uwanja wa Monumental kujaa maji.

Maafisa wa chama cha soka nchini Argentina, walionekana wakihangaika kunusuru hali ya sehemu ya kuchezea ya uwanja huo, lakini juhudi zao zilishindikana na kufanyika maamuzi ya mpambano huo kuahirishwa.

Hata hivyo taarifa zilizopatikana muda mchache baadae zilithibitishwa kwamba, mchezo huo utachezwa hii leo jioni kwa saa za Amerika ya kusini kwenye uwanja wa ule ule wa Monumental.

Miamba hiyo miwili itakutana, ikiwa ni sehemu ya kuendelea na kampeni za kusaka tiketi ya kucheza fainali za kombe la dunia za mwaka 2018, ambazo zitafanyika nchini Urusi.

Timu hizo zilianza vibaya kampeni za kusaka njia ya kuelekea nchini Urusi kwa mwaka 2018, ambapo kwa upande wa Brazil walikubali kupoteza mchezo dhidi ya Chile kabla ya kuibuka na ushindi dhidi ya Venezuela ili hali kwa upande wa Argentina, mpaka sasa wameshindwa kufunga bao hata moja licha ya kujikusanyia point moja iliyotokana na matokeo ya sare ya bila kufungana dhidi ya Paraguay.

Katika mchezo wa kwanza Argentina walikubali kufungwa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Ecuador.

Katika mchezo wa hii leo kikosi cha Brazil kinatarajiwa kupata chagizo la ushindi kutoka kwa mshambuliaji wa FC Barcelona Neymar ambaye amerudi baada ya kutumikia adhabu ya kufungiwa, huku Argentina wakiendelea kuwa wapweke kufuatia manguli wao Lionel Messi, Sergio Aguero na Carlos Tevez  kuendelea kujiuguza majeraha.

Unyama: Msichana Asimulia Alivyobakwa Zaidi Ya Mara 43,000
Kombe La Dunia 2018, Burundi Yakwama Nyumbani