Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amemtakia maisha mema aliyekuwa mjumbe wa kamati kuu ya chama hicho Edward Lowassa baada ya kurejea CCM.

Mbowe ambaye yupo gereza la Segerea ambapo anatumikia adhabu yake ya kukiuka masharti ya dhamana kutokana na kesi yake inayomkabili, amesema kuwa safari ya mabadiliko lazima ipite katika vikwazo vingi na si wote watakaofika mwisho wa safari hivyo wapo watakaoishia njiani.

Amesema kuwa Julai 2015, walimpokea Edward Ngoyai Lowassa katika chama chao na baadae kupitishwa na vikao vya chama kuwa mgombea wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini machi 01, 2019, Lowassa ametangaza kurudi katika chama chake cha zamani Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Wana-CHADEMA tunapotafakari jambo hili rejeeni kauli yangu ya wakati wote inayobeba falsafa yetu ya mabadiliko, kwamba safari ya kusaka mabadiliko ni sawa na safari ya treni kutoka Dar es salaam kuelekea Kigoma, wapo wanaoanza na safari mwanzo wa safari na wapo wanaoanzia katikati, pia wapo wanaoteremka njiani na wapo wanaoendelea na safari hadi mwisho, wote hao ni abiria, cha msingi kwetu hapa ni kuhakikisha safari yetu inaendelea, na ni imani yangu na matumaini yangu kwamba mtakubaliana na mimi kuwa safari yetu inaendelea,”amesema Mbowe

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi CUF, Prof. Ibrahim Lipumba amesema kuwa Lowassa amerudi CCM bila aibu, wakati Mbowe bado yupo gerezani na hakufikiria wenzake anawaachaje.

Hata hivyo, Lowassa ambaye pia ni Waziri Mkuu mstaafu Machi mosi alitangaza kurejea CCM na kudai kuwa aliondoka kutokana na sababu zilizokuwa nje ya uwezo wake.

 

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 4, 2019
Hivi ndivyo mashindano ya Kili Marathon yalivyofana