Kikosi cha Mwadui FC leo kinaikaribisha Simba SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara utakaounguruma kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.

Mwadui wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu ya kuchapwa na SImba mabao 3-0 katika mechi wa mzunguuko wa kwanza, Septemba 17, mwaka jana Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.

Kichapo hicho kilitolewa wakati Simba SC bado inafundishwa na kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog, kabla ya kumfukuza na kumleta Mfaransa Pierre Lechantre.

Simba SC itaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa dhamira ya kushinda na kuendelea kujiweka vizuri kwenye uongozi wa Ligi Kuu katika harakati za kutwaa ubingwa wake wa kwanza baada ya miaka mitano.

Kwa sasa, Simba SC wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 41, wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 37, wakati Azam FC wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao 34.

Ligi Kuu itaendelea kesho, Lipuli FC wakiwa wenyeji wa Azam FC Uwanja wa Samora mjini Iringa, wakati keshokutwa kutakuwa na michezo miwili, Njombe Mji FC watawakaribisha Majimaji ya Songea Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe na Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa Singida United Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.

Mchezo mmoja tu itachezwa Jumapili, Mbeya City wakiikaribisha Stand United Uwanja wa Sokoine, wakati Jumatatu kutakuwa na mechi mbili pia, Tanzania Prisons na Mwadui FC Uwanja wa Sokoine na Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro.

Video: Dkt. Tulia afunguka mazito kuhusu matibabu ya Lissu
Penzi la Diamond na Zari latia nanga, Zari aanika madudu ya Diamond