Makamu Mwenyekiti wa Young Africans Fredick Mwakelebela amesema Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison ni mchezaji mwenye uwezo kisoka, na klabu yoyote nchini inahitaji kufanya naye kazi.

Mwakalebela ametoa kauli hiyo, huku Young Africans ikitajwa kuwa kwenye mpango wa kumrudisha Kiungo huyo kufuatia mkataba wake na Simba SC kutarajia kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.

Akizungumza na TV3, Mwakalebela amesema kwa sasa hawezi kuzungumza lolote kuhusu mchezaji huyo kurudi Young Africans lakini amekua akimfuatilia na kuridhishwa na uwezo wake kisoka.

Amesema pamoja na Morrison kutajwa kwa mtovu wa nidhamu katika kipindi hiki, bado haimpotezei sifa yake ya kuwa mchezaji bora anayejua kutumia vizuri kipaji chake.

“Ana uwezo mkubwa sana, anajua namna ya kutumia kipaji chake anapokua uwanjani, binafsi ninampenda sana, Swala la Morisson hatuwezi kuliongelea sasa hivi, lakini ni mchezaji ambaye kila klabu ingependa kuwa nae, ni mchezaji mzuri ila nidhamu yake tu ndiyo shida”

Hata Hivyo Mwakalebela amewashangaza wengi, baada ya kusema Morrison alipokua Young Africans hakuwahi kuonyesha utovu wa nidhamu wa aina yoyote, na badala yake alikua sehemu ya wachezaji waliokua wanafuata msingi na kanuni iliyowekwa klabuni hapo.

“Bernard Morrison alipokuwa Young Africans hakuwahi kuonesha utovu wa nidhamu, kuna misingi na kanunu alikua anaifuata, ni basi tu alishawishika akaihama klabu yetu, tulijitahidi kupambana FIFA, CAF hatukufanikiwa.”

“Siwezi kuzungumza sana kuhusu kuja kwake Young Africans kwa sababu halijafanyika hilo jambo, ni vyombo vya habari vimekua vinalizungumzia hilo jambo. Lakini nisisitize tu, ni mchezaji mzuri mwenye kipaji kikubwa.” ameongeza Mwakalebela

Morrison alisajiliwa Simba SC mwanzoni mwa msimu uliopita, baada ya kumaliza mkataba wake na Young Africans licha ya kuibuka kwa sintofahamu kati yake na viongozi wa klabu hiyo ambayo ilimleta nchini wakati wa Dirisha Dogo la Usajili msimu wa 2019/2020.

Mwakalebela aishutumu Simba SC Ligi Kuu
Ahmed Ally arudisha majibu Young Africans