Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe ambaye ameapishwa leo na rais John Magufuli kushika wadhifa huo amewaomba wadau na wananchi kwa ujumla kumpa muda.

Akiongea na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuapishwa, Dkt. Mwakyembe ambaye alikuwa waziri wa wizara mbalimbali katika serikali ya awamu ya nne amesema kuwa anafahamu changamoto nyingi katika mfumo wa sheria ya nchi akiwa kama mwananchi. Hivyo, ameomba kupewa muda ili atakapoingia ofisini azifanyie kazi changamoto hizo.

Dk. Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria aliyebobea, alieleza kuwa mfumo bora wa sheria ya nchi ni kitu muhimu katika kipindi hiki ambacho serikali imeamua kufanya mabadiliko makubwa ya kimfumo.

“Tuko katika kipindi cha mageuzi makubwa ya uchumi wetu na masuala ya kijamii na kiuchumi, kwahiyo masuala ya kisheria yatajitokeza sana hapo. Ndio maana nasema… sawa ni eneo langu kisheria lakini changamoto ziko nyingi ambazo lazima tukabiliane nazo ili nchi yetu iende kwa kasi ambayo rais wetu ameanza nayo,”alisema.

Akizungumzia mchakato wa Katiba Mpya uliokuwa ukiendelea katika serikali ya awamu ya nne, Dk. Mwakyembe amesema suala hilo litakamilishwa kutoka pale lilipoishia.

“Mheshiwa rais ameshalielezea vizuri sana hilo kwamba katika kipindi chake tutalifanyia kazi, na hatukuishia pabaya tuliishia pazuri tu, tutalitekeleza, muda utafika na naamini tutalikamilisha vizuri tu,”aliongeza.

Roger Federer Kucheza Na Martina Hingis
Rais Magufuli Aapisha Baraza La Mawaziri