Kufuatia ongezeko kubwa la mmomonyoko wa maadili ya Kitanzania, Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeamua kupitisha rasmi kanuni za maudhui ya mtandaoni, redioni na kwenye runinga, Pia vyombo vya habari vya magazeti navyo vikivunja sheria kwa kutozingatia weledi wa taaluma za kuchapisha habari zenye makosa ya kitaaluma.

Hayo yaliwasilishwa Bungeni na Waziri wa wizara hiyo, Dk. Harrison Mwakyembe wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara yake.

Pia amesema kanuni hizo mpya zilizotungwa chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta ya Mwaka 2010, zinazuia mitandao, runinga na redio kusambaza kauli chafu, matusi, picha za utupu na zenye maudhui yasiyofaa kwa watoto.

“Pia mitandao, redio na luninga kwenye zitaingizwa kwenye mfumo rasmi wa kutambulika kisheria na kuwajibika kulipa. Zinamtaka kila mtumiaji mitandao awe na namba yake ya siri ili wajanja wasitumie kiurahisi chombo chake cha mawasiliano kutenda matendo hasi kinyume na sheria,” alisema Dkt Mwakyembe.

Alieleza kuwa kanuni hizo pia zinaweka muda maalumu kwa picha nyongevu za filamu au muziki wenye maneno yasiyo mazuri kwa watoto, zionyeshwe kwenye runinga katika muda maalumu.

“Tuliweka muda huo maalumu kuanzia saa nne usiku hadi saa 11:30 asubuhi, lakini wadau wamekuwa wakali, wanadai picha na nyimbo hizo zirushwe kuanzia saa 6:00 usiku wakati watoto wamelala na mwisho saa 11:00 asubuhi, kabla watoto hawajaamka,” alifafanua.

Alisema pamoja na kupitisha kanuni hizo ambazo tayari zimeanza kufanya kazi, pia wizara hiyo itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kikabiliana na changamoto hiyo ya mmomonyoko wa maadili ya kitanzania. Alisema katika kufanikisha hilo, itaendelea kuhamasisha utengenezaji na uzalishaji wa maudhui ya ndani yanayozingatia maadili, mila na desturi za Mtanzania.

UN kuupigia kura mgogoro wa Sahara Magharibi
Nondo atunukiwa tuzo