Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe amewaonya askari wa Jeshi la Polisi kutotumia nguvu kupita kiasi pale wanapowakamata watuhumiwa.

Harrison Mwakyembe

Waziri huyo anaeendelea na ziara yake Kanda ya Ziwa Victoria, amesema kuwa utafiti uliofanywa hivi karibuni umebaini kuwa polisi wengi hutumia nguvu kupita kiasi wanapowakamata watuhumiwa wa makosa mbalimbali.

Aliongeza kuwa utafiti huo umebaini pia kuwepo kwa tabia ya baadhi ya askari polisi wanaowabambikia kesi wananchi.

“Utafiti huo umeonesha pia kuwa wapo baadhi ya polisi ambao wamekuwa wakiwabambikia kesi wananchi. Baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamika kuwa mashtaka dhidi yao ni tofauti,” alisema Mwakyembe alipokuwa akizungumza na Kitengo cha Mahakama katika kanda hiyo.

Kadhalika, alisema kuwa kuna baadhi ya wananchi ambao wamekuwa wakikataliwa kupewa dhamana na polisi kinyume cha sheria.

Akitoa mfano, alisema kuwa kuna mtuhumiwa katika gereza la Keko ambaye amenyimwa dhamana kwa miaka 13 ingawa alishatimiza vigezo vya dhamana hiyo na kwamba polisi wamekuwa wakidai kuwa upelelezi dhidi ya kesi yake bado haujakamilika.

Dk. Mwakyembe aliwataka polisi kuhakikisha kuwa wanatenda haki kwa wananchi hasa  pale wanapowashikilia.

 

Makonda amkataa Mkurugenzi wa Jiji, abaini Wizi Mkubwa
DART YAHIMIZWA KUELIMISHA WAKAZI WA DAR