Waziri Wa Habari, Sanaa Utamaduni Na Michezo Harrison Mwakyembe ameliibua upya sakata la kiungo mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison ambaye juma lililopita aliishinda klabu ya Young Africans, mbele ya kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya shirikisho la soka nchini Tanzania (TFF).

Morrison aliwashtaki viongozi wa Young Africans mbele ya kamati hiyo kwa madai ya saini yake kugushiwa kwenye mkataba ambao ulidaiwa ulikua na makubaliano ya pande hizo mbili kwa muda wa miaka miwili.

Waziri Mwakyembe amesema maamuzi ya hukumu ya sakata hilo hayakumfurahisha, kutokana na kuamini TFF kupitia kamati yake hawakupaswa kuchukua muda mrefu kutangaza hukumu kama ilivyokua.

 “Halijanifurahisha kwa sababu limetupotezea muda mwingi sana, badala ya kufanya mambo mengine ya kuendeleza michezo, tunalumbana kuhusu mtu mmoja!”

“Sio kwa TFF, lakini limetoa changamoto kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kwamba waliangalie hilo, kwa sababu linavyozidi kuendelea linaingilia mpaka sera za michezo ya nchi.” amesema Waziri Mwakyembe alipohojiwa na Televisheni ya Taifa (TBC).

Katika hatua nyingine waziri huyo mwenye dhamana ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, amedai kuwa baada ya sakata hilo, ni dhahir wadau wa soka hususan wanachama na mashabiki wa Simba SC na Young Africans, wamekua na mvutano wa hapa na pale huku viongozi wa klabu hizo wakiwa kwenye mbinu chafu za kukomoana.

“Hili la Morrison limenifundisha kitu kimoja, hebu tuangalia upya hasa kwa timu hizi mbili zinapoleta wachezaji, Je? Ziruhusiwe kunyang’anyana wachezaji hapa hapa, ama huyo mchezaji kama anaondoka anapaswa kurudi kwao kwanza.”

“Nimewaambia BMT waande kulitafakari hilo, ni kitu muhimu sana, lakini kuingilia kati suala la Morrison siwezi kwa sababu sio la kisera ni suala la kiufundi, hivyo TFF na wadau wengine wa soka watalimaliza.”

Juma lililopita Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Elias Mwanjala alisema Bernard Morrison ameshinda kesi yake dhidi ya Young Africans na ataendelea kuwa mchezaji huru, baada ya mapungufu kukutwa kwenye mkataba baina pande hizo mbili.

Kamati pia ilimpeleka Morrison kwenye Kamati ya Maadili ya TFF, Kwa kuingia mkataba na timu nyingine huku Kesi ya msingi ikiwa inaendelea.

Rais wa Mali ajiuzulu, jeshi lachukua madaraka
Exclusive: 20 Percent afunguka tetesi za kutumia unga, ‘nasikia joto, baridi’