Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe  amesema kuwa serikali imeimarisha sekta ya Mahakama nchini ambapo imeanzisha kamati ya maadili ya mahakama katika kila wilaya nchi nzima  ili kusimamia upotofu wa maadili katika mahakama hizo.
Dkt. Mwakyembe  amesema  hayo  wakati wa kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoandaliwa na Idara ya Habari-MAELEZO kwa kushirikiana na  TBC 1 ambapo alisema Serikali imeamua kuanzisha kamati hizo ili zipokee upotofu wa maadili unaofanywa na baadhi ya watumishi wa mahakama ambao sio waaminifu hali ambayo inaharibu sifa ya chombo hicho cha kutoa haki.
“Tumeanzisha kamati hizi katika kila wilaya ili zipokea  upotofu wa maadili kwa upande wa mahakama, sasa wananchi wanaweza kwenda kutoa malalamiko yao kwenye kamati hizo ili yaweze kufanyiwa kazi na hatua  zitachukuliwa kwa wale watakaokutwa na makosa”.
“Kamati hizo zinazoongozwa na wakuu wa wilaya zinaundwa na wajumbe mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini ili kuwapa wananchi fursa nzuri  ya kuweza kutoa malalamiko yao”. Alisema Dkt. Mwakyembe.
Aidha, Dkt. Mwakyembe alisema kuwa kwa sasa Serikali imeendelea kuwa na mikakati kadhaa ya kuimarisha sekta ya Mahakama nchini, ambapo inaendelea kukamilisha maandalizi ya mfumo wa divisheni ya mahakama ya rushwa na ufisadi ili itakapoanza iweze kufanyakazi bila matatizo.
“Tunaendelea kujiandaa na idara zote zinazohusika  katika  mahakama hiyo, ili ziweze kufanya kazi vizuri, tumeweka vigezo vya kesi zitakazosikilizwa huko na hakutakua na kesi za mwaka juzi au muda mrefu kwa kuwa zitasikilizwa kwa wakati”.  Alisisitiza Dkt. Mwakyembe.
Akizungumzia wananchi wanaoshindwa kumudu gharama za huduma za kisheria zinazotozwa na mawakili au wanasheria mbalimbali, Dkt. Mwakyembe alisema kuwa Serikali imeandaa mswaada ambao utapelekwa Bungeni ili kutunga Sheria itakayosaidia kutatua changamoto hiyo.
Dkt. Mwakyembe  aliongeza kuwa  serikali imeendelea kushirikiana na vikundi vya harakati na asasi za kirai zaidi ya 290 vyenye wataalamu wa sheria 2500 nchi nzima ili kupanua wigo wa masuala ya sheria, pamoja na kuandaa mfumo wenye tija kwa taifa utakaosaidia kuwafikia na kuwasaidia wananchi wengi  hasa waliopo maeneo ya vijijini ili kupata msaada wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali hasa mirathi ya ndoa na ardhi.
Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Mahakama kwa wingi kwa ngazi mbalimbali pamoja na kuwaandaa vijana wengi kutoka vyuo vikuu kila mwaka ambao watafanyakazi katika mahakama mbalimbali nchini.

Magufuli ataka Shein amuadhibu Maalim Seif, aeleza ambacho angemfanya kwa kugoma kumpa mkono
RPC awatoa wananchi hofu ya Ugaidi, ni baada ya Hostel kuvamiwa Tanga