Kipande cha video kilichosambaa kwenye mitandao ya kijamii kikiwaonesha walimu waliobainika kuwa wanafunzi wa vyuo wakimshambulia mwanafunzi wa kiume imepelekea walimu hao pamoja na mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari ya kutwa ya Mbeya, Magreth Haule kutumbuliwa.

Waziri wa Elimu na mafunzo ya ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ametangaza kuwafukuza vyuoni walimu hao watatu walioonekana wakimpiga kwa kumchangia mwanafunzi huyo wa kidato cha tatu aliyetajwa kwa jina la Sebastian Chinguku.

Walimu hao waliokuwa wakifanya mafunzo kwa vitendo shuleni hapo wametajwa kuwa ni Frank Msigwa na John Deo (Chuo Kikuu cha Dar es Salaam) pamoja na Sanke Gwamaka (Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere).

“Hadi sasa walimu wote wa shule hiyo akiwemo mwalimu mkuu wanashikiliwa ktk kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa maelezo,” Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla anakaririwa.

Aidha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene ameagiza Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Magreth Haule kuvuliwa madaraka mara moja baada ya kubainika kuwa alitaka kuficha tukio hilo na hakuchukua hatua stahiki.

Imeelezwa kuwa Septemba 28 mwaka huu, mwalimu Frank alitoa zoezi la somo la Kiingereza ambapo baadhi ya wanafunzi hawakufanya akiwemo mwanafunzi huyo (Sebastian). Mwalimu huyo alimpiga kofi Sebastian ambaye alihoji sababu za kufikia uamuzi huo na kisha kukabana koo na mwalimu huyo.

Walimu walimchukua Sebastian na kumpeleka kwenye ofisi ya walimu kisha kumshambulia kwa fimbo na makofi makali usoni. Video ya tukio hilo ilichukuliwa kwa njia ya simu na mwalimu  mmoja ambaye anasikika kwenye video hiyo akisema “mwacheni mtamuumiza”.

Zitto awasifu Ukawa lakini...., asema ‘neno’ kuhusu CUF
DC Staki ashiriki shughuli za kijamii