Nahodha na Beki wa Young Africans Bakari Nondo Mwamnyeto amefichua siri ya ushindi walioupata dhidi ya KMC FC leo Jumanne (Oktoba 19).

Young Africans imechomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidii ya KMC FC waliokua nyumbani Uwanja wa Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma.

Mwamnyeto amesema kwa asilimia 100 wamefuata maelekezo ya Benchi lao la ufundi, na ndio maana wamefanikiwa kuondoka na alama tatu muhimu katika Uwanja wa ugenini.

Amesema Kocha Nabi pamoja na Msaidi wake Cedrick Kaze waliwahimiza kucheza kwa nguvu katika dakika 15 za kwanza, na walifanikiwa kupata mabao mawili yaliyowapa alama tatu muhimu.

“Kocha alituhimiza tucheze kwa bidii na maarifa dakika 15 za kwanza, na kweli tulifanya hivyo na tukafanikiwa kupata mabao yaliyotupa ushindi leo tukiwa katika uwanja wa ugenini,”

“Tunashukuru tumeyafanyia kazi maagizo ya kocha wetu na msaidi wake, na hii inaendelea kutujengea hali ya kujiamini kila tunapokuja kushindana uwanjani.” amesema Mwamnyeto.

Mabao ya Young Africans dhidi ya KMC FC yamefungwa na Fiston Mayele na Feisal Salum dakika ya 06 na 11 kipindi cha kwanza.

Kuhusu ujumbe kwa Mashabiki na Wanachama waliojitokeza Uwanja wa Majimaji kuwashangilia Mwamnyeto amesema: “Tumefarijika kwa kuja kwao hapa, na hii ndio timu yao, waendelee kutupa ushirikiano na sisi hatutawaangusha.”

Ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC FC, unaipeleka Young Africans kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha alama 09.

Namungo FC yazamishwa Azam Complex Chamazi
Sikutegemea "Essence":Wizkid