Mtume na Nabii, Boniface Mwamposa amezungumza kwa mara ya kwanza na vyombo vya habari kuhusu tukio la watu 20 kupoteza maisha katika kongamano lake mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, wakijaribu kukanyaga ‘mafuta ya upako’, Februari Mosi, 2020.

Mwamposa ambaye alishikiliwa kwa muda na Jeshi la Polisi na baadaye kuachiwa kwa dhamana, amezungumza na kipindi cha Chomoza cha Clouds TV muda mfupi kabla ya kuanza ibada ya Jumapili katika Viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa anatambua wapo maadui katika tukio kama hilo na ndio sababu mambo mengi yamezungumzwa, lakini yeye anamuachia Mwenyezi Mungu amsimamie.

“Unajua linapofika jambo kama hili lazima kila mtu ataongea la kwake, katika huduma kama hizi kuna marafiki na kuna maadui, lazima ukubali,” alisema Mwamposa. Aliongeza, “Lakini sasa hatuwezi kusema mengi kwa sababu tayari Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama vinachunguza jambo hili nikiongea mengi nitakuwa navuruga uchunguzi wao.”

“Nachofahamu kuwa jambo hili lilitokea nikiwa nimeshatoka nakimbilia Dar es Salaam kwenye Kongamano [lingine], na niliwahi pia ili niwatulize watu isije ikatokea ghasia nyingine Dar es Salaam. Nashukuru viongozi wangu wa huduma walivyolisimamia jambo hili, na Serikali inaendelea kutafuta ukweli na nafikiri baada ya uchunguzi kila kitu kitajulikana,” alisema.

Mwamposa alitoa pole kwa familia ndugu na Taifa kwa ujumla kutokana na tukio hilo, akaeleza kuwa anaamini Mungu atawasimamia. Alisema aliamua kwanza kukaa kimya kwa sababu lilikuwa jaribio kubwa ambalo limeumiza Taifa kwa ujumla, hivyo alimuachia Mungu asimamie.

Aidha, kiongozi huyo wa dini alieleza kuwa ameamua kusitisha ratiba ya makongamano yake ya kukanyaga mafuta ya upako kutokana na tukio hilo, lakini yataendelea baada ya muda

“Kwa mfano leo ilikuwa kuwe na kongamano kubwa la kukanyaga mafuta, lakini kutokana na shida iliyotokea tumeyasimamisha yote kutaka utulivu na kuomba Mungu atupatie neema ya kupanga mipango upya,” alisema.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Miseme, Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro alituma watalaam wa uchunguzi wa sayansi ya jinai ili kusaidiana na timu nyingine ya jeshi hilo mjini Moshi.

Mwamposa na wenzake saba wanapaswa kuripoti polisi kwa utaratibu waliopewa wakati uchunguzi ukiendelea.

Sababu 5 zisizoepukika mtoto mchanga kulialia usiku
Fanya haya uonekane mrembo siku zote