Tofauti za kisiasa zilizopo nchini zisivuruge nuru ya amani iliyojengwa tangu enzi za Serikali ya Awamu ya Kwanza ambapo siasa za nchi zililenga katika umoja, amani na ujenzi wa Taifa imara, anaonyesha mmoja wa walimu wa diplomasia nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia nchini (CFR), Dkt. Bernard Achiula wakati wa mahojiano na Mwandishi wa habari hii kuhusu hali ya siasa nchini kwa sasa na ushiriki wa watanzania kwa ujumla katika kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Tano katika utatuzi wa changamoto za kimaendeleo badala ya kuanzisha tabia za vurugu na maandamano.

Dkt. Achiula amesema kuwa uwepo wa amani nchini unachangia katika kuvutia wawekezaji  nchini, kukuza utalii wa ndani, kuvutia wahisani kutoa misaada kwa kuchangia katika uanzishaji na uendelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hivyo kila raia nchini bila kujali itikadi yake ya dini wala chama ana budi kuilinda amani iliyopo.

“Tofauti za kisiasa zipo katika kila nchi kulingana na mitazamo tofauti iliyopo ila kinachotakiwa ni kuweka taifa mbele kwa manufaa ya nchi, watanzania tunatakiwa kuwa wazalendo ili kuimarisha umoja na amani iliyopo kwani vitu hivi vinategemeana na hatimaye kuiwezesha Serikali ya awamu ya tano kuwatumikia wananchi kwa kuwaletea maendeleo.

“Tofauti hizo zisiwe chachu ya kuvuruga amani tuliyonayo bali watanzania kwa ujumla tunatakiwa kuitunza amani hii iliyojengwa tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere ili kuweza kuvutia wawekezaji na  utalii katika nchi yetu” alifafanua Dkt Achiula.

Alisema kuwa haoni sababu kwa vyama vya siasa nchini kuandaa maandamano yanayolenga kuvuruga amani iliyopo kwani kikubwa kinachotakiwa kwa wananchi ni misingi mikuu ya maendeleo ikiwemo elimu, afya na huduma bora mbalimbali  ambapo Rais Magufuli ameanza kuvifanyiakazi.

Akizungumza kuhusu Balozi zetu nje ya nchi Dkt Achiula aliwashauri mabalozi hao kuzidi kuitanganza nchi yetu ya Tanzania ili kuweza kuvutia wawekezaji, utalii na biashara ili kusaidia katika ukuuaji wa sekta ya viwanda ambapo Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuipeleka nchi katika uchumi wa viwanda.

Akizungumzia utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano Dkt Achiula amesema kuwa Rais Dkt. Magufuli amejikita katika kutatua changamoto zinazolikabili taifa kwa muda mrefu ikiwemo kupiga vita rushwa, kuongeza ukusanyaji mapato kwa kuwabana wakwepa kodi, kubana matumizi ikiwa nia ni kuimarisha uchumi wa nchi na kuipeleka nchi kwenye uchumi wa Kati

Lukuvi;Tumejipanga Kuipima Ardhi Nchi Nzima
Mhariri Mkuu BAKITA Awaasa Watanzania Kutunza Lugha Za Asili Ili Kuboresha Kiswahili