Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mwanafunzi wa kidato cha tano wa shule ya Sekondari ya Mawenzi, Moshi mkoani Kilimanjaro, amejifungua katika choo cha shule hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka shuleni hapo, mwanafunzi huyo ambaye jina lake limehifadhiwa alimuacha mwanaye kichanga katika choo cha shule hiyo baada ya kujifungua salama alipokwenda kujisaidia majira ya saa kumi alfajiri.

Wanafunzi wenzake walifanikiwa kubaini tukio hilo na kutoa taarifa kwa uongozi wa shule.

“Alichukua muda mrefu akiiwa chooni, hii ikawafanya wenzake wamtilie shaka na kuanza kumfuatilia. Walimdadisi hakusema chochote, baada ya kumbana alieleza kuwa amejifungua,” chanzo kinakaririwa na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa.

Baada ya kubainika, alipelekwa katika hospitali ya St. Joseph ambapo imeelezwa kuwa hali yake na mwanaye vinaendelea vizuri.

Akizungumzia kuhusu tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Koka Moita alisema kuwa wamepata taarifa za kuwepo kwa tukio hilo, lakini halijaripotiwa katika kituo chochote cha polisi.

Tukio hilo limewashangaza wengi hususan namna ambavyo mwanafunzi huyo aliweza kukaa na ujauzito wa miezi tisa bila kubainika, na alivyoweza kusajiliwa kidato cha tano ili hali ana ujauzito kwani wanafunzi wote wa kike hupimwa afya zao kabla ya kudahiliwa.

Uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kupitia kwa Kaimu Mkurugenzi wake, Uhuru Mwembe umesema meanza uchunguzi wa tukio hilo.

Polisi waingilia kati mafuriko ya watu soko 'halali' la bangi
Video: JPM akutana na Taifa Stars Ikulu, akabidhi milioni 50

Comments

comments