Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Kilimo cha Jomo Kenyatta aliandika mpango wake kwenye ukurasa wake wa Facebook kabla ya kutekeleza tukio la kuruka ukuta wa Ikulu ya Kenya akiwa na kisu, imebainika.

Juni 10, 2019 majira ya jioni, Brian Kibet Bera alijaribu kuruka ukuta wa Ikulu ya nchi hiyo. Alipozuiwa na walinzi alitoa kisu alichokuwa nacho hali iliyowalazimu walinzi hao kumpiga risasi iliyomjeruhi bega la kushoto.

Hata hivyo, baada ya kukamatwa, ukurasa wake wa Facebook ulibainika kuwa na mpango wote wa uvamizi wake Ikulu ikiwa ni pamoja na sababu.

Juni 7, 2019 alielezea kuwa anapanga kuingia Ikulu kwa lengo la kumshambulia Rais Uhuru Kenyatta kwa madai kuwa Serikali yake imenyang’anya ardhi aliyoachiwa na babu zake.

“Nitaenda Ikulu nikiwa na panga, (au ni wapi naweza kumpata Rais Uhuru Kenyatta?). Naenda kumfyeka Rais Uhuru Kenyatta na wezi wenzake kwa sababu wameiba ardhi ambayo Mungu aliwapa wazee wangu,” aliandika kwa lugha ya Kiingereza kwenye ukurasa wake wa Facebook.

Jana, baba yake mzazi Hussein Mohammed alifanya mahojiano maalum na Citizen TV na kueleza kuwa mwanaye ana matatizo ya akili. Aliiomba Serikali kumuachia huru na kumsadia matibabu ya akili.

“Huyu kijana mdogo, mwanangu… anaweza kutoa mchango mkubwa kwa Taifa la Kenya kama atatibiwa,” alieleza kwenye mahojiano maalum na kituo hicho.

Kijana huyo ni mwanafunzi wa mwaka wa tano anayesomea Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Kilimo cha Jomo Kenyatta.

Mexico yapiga mnada ndege ya Rais kudhibiti uhamiaji haramu
LIVE: Yanayojiri Bungeni jijini Dodoma leo Juni 13, 2019