Wanafunzi 19 wamekufa na wengine makumi wamejeruhiwa baada ya mwanafunzi mwenzao kuwafyatulia risasi katika chuo cha eneo la Crimea nchini Urusi.

Mwanafunzi huyo mwenye umri wa miaka 18, anadaiwa kupita katika vyumba kadhaa vya bweni la wanafunzi pamoja na mgahawa wa chuo hicho akifyatua risasi hovyo.

Mshambuliaji huyo ambaye ametajwa kwa jina la Vladislav Roslyakov, alijiua baada ya kufanya mauaji hayo, kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na kamati maalum ya vyombo vya ulinzi vya Urusi.

Vyombo vya ulinzi na usalama vimeeleza kuwa mbali na shambulizi hilo pia milio ya milipuko kadhaa ilisikika katika eneo hilo. Wapelelezi wa tukio hilo wameeleza kuwa walibaini kuwepo kwa kilipuzi kimoja kwenye mfuko wa mshambuliaji huyo.

Taarifa za awali zililitaja tukio hilo kama shambulizi la kigaidi, lakini wapelelezi wa Urusi walieleza kuwa halikuwa na uhusiano na ugaidi.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema kuwa shambulizi hilo kama janga na kutoa salamu zake za rambirambi kwa wahanga wa tukio hilo.

Urusi ilijitwalia eneo la Crimea kutoka Ukraine mwaka 2014 na kulitangaza kuwa sehemu ya ardhi ya nchi hiyo, hatua iliyopingwa na nchi nyingi za Magharibi.

Marekani yafyeka makumi ya wapiganaji wa Al-Shabaab
Polisi aliyesema ‘Kidumu Chama Cha Mapinduzi’ apigilia msumari