Mwanafunzi wa darasa la tatu wa Shule ya Msingi Itumbili, Nzega mkoani Tabora, Tatu Maganga (9) amekutwa amefariki baada ya kujinyonga kwa kutumia shati lake la shule.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley amesema tukio hilo limetokea juzi majira ya saa 8 mchana katika kijiji cha Kikonoka wilayani Nzega.

Ameeleza kuwa taarifa za kifo cha mtoto huyo zilifikishwa kituo cha polisi kata ya Mambali na Mkuu wa kituo hicho, ndipo Koplo Shaban Shaban akaenda eneo la tukio na kukuta mwili wa mwanafunzi huyo ukiwa umening’inia kwenye mwembe.

Kutokana na uchunguzi wa polisi kwa kushirikiana na madaktari wa Zahanati ya Mambali wakiongozwa na Dkt. Felix Manjwa, wamebaini mwanafunzi huyo alijinyonga kwa kutumia shati lake la shule.

Kamanda Nley amesema baada ya uchunguzi wao kukamilika mwili wa mwanafunzi huyo ulikabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya kuendelea na taratibu za mazishi, na kuongeza kuwa licha ya kuwapo kwa viashiria vyote vinavyoonyesha mtoto huyo kajinyonga, bado Jeshi la Polisi wataendelea na uchunguzi wa kina.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Itumbili, Mrisho Masanja amesema tukio hilo limekatisha ndoto za mwanafunzi huyo na kuwataka wazazi kuwa karibu na watoto wao na kuwasikiliza wanapokuwa na manung’uniko yoyote.

Naye Mkuu wa shule ya msingi Itumbi, Yona Athnas, amesema siku ya tukio binti huyo alikuwa darasani na hakuonesha kuwa na tatizo lolote na walimu au wanafunzi wenzake na kwamba mara ya mwisho aliondoka shuleni saa nne asubuhi wakati wa mapumziko.

 

 

 

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 10, 2019
Spika azungumzia hatma ya sakata la CAG na Mdee

Comments

comments