Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia mwanafunzi wa kidato cha pili anayesoma shule ya Sekondari St Apostos, Yela Sylvester maarufu Cosmas (17), kwa kosa la kudanganya wazazi wake kuwa ametekwa ili ajipatie fedha.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Jumanne Muliro amewaeleza waandishi wa habari kuwa tukio hilo lilitokea April 27 mwaka huu saa nne usiku katika Mtaa wa Mahah wilayani Magu.

Ameeleza kuwa baada ya kijana huyo kusindikizwa kwenda shule na mzazi wake hadi kituo cha mabasi cha Buzuruga jijini Mwanza na alipakizwa kwenye basi la Shelatoni linalofanya safari zake  kati ya Mwanza na Geita.

Lakini kijana Cosmas hakwenda shule na badala yake alitumia simu namba 0689447247 na kutuma ujumbe mfupi kwa baba yake, huku akificha laini yake ya zamani ya simu kwa madai kuwa alikuwa ametekwa kwa kujipatia fedha.

“Kwenye ujumbe aliomtumia baba yake, alidai kuwa endapo wasipotuma fedha hizo atapelekwa na watekaji nchini Zambia kufanya kazi kitendo ambacho ni kinyume cha sheria” Amesema kamanda Muliro.

Na kueleza kuwa Polisi walifanya ufuatiliaji wa taarifa hizo za kutekwa kwa mwanafunzi huyo na kumtia nguvuni akiwa salama, Lamadi wilayani Magu akiwa na laini ya simu aliyotumia kumdanganya baba yake kuwa alikuwa ametekwa.

Kamanda Muliro amesema wanaendelea kumhoji na uchunguzi ukikamilika atafikishwa mahakamani ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yake.

 

JPM awataka wafanyakazi kuwa wavumilivu, 'mishahara itapanda'
Video: TUCTA watoa ombi kwa Serikali, JPM awajibu

Comments

comments