Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Iringa, Petronel Mwanisawa (22) amefariki dunia kwa kunyongwa na mpenzi wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma Bwire amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba wanamshikilia mtuhumiwa, Prudence Patrick (21), ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika chuo hicho.

Mwanafunzi Petronila Mwanisawa aliyeuawa

Kamanda Bwire amesema tukio hilo limetokea Juni 1, mwaka huu maeneo ya Kihesa ambapo siku ya tukio marehemu hakurudi nyumbani kwao jambo ambalo si kawaida yake, hivyo wazazi wake waliingiwa na hofu na kuanza kumtafuta.

“Marehemu alikuwa anaishi na wazazi wake, na huyu mtuhumiwa yeye alikuwa amepanga. Kwa hiyo siku ya tukio alitoka kwenda chuo, lakini mpaka usiku akawa hajarudi, ndipo wazazi walianza kupata wasiwasi, wakampigia simu rafiki yake lakini hawakufanikiwa,” amesema Kamanda Bwire

Taarifa za tukio hili ziligundulika baada ya mtuhumiwa mwenyewe kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa Mzazi wa marehemu akisema alikuwa na Petronel na kwamba amefariki.

Prudence amekamatwa katika kituo kikuu cha mabasi cha Iringa akiwa anatoroka baada ya mauaji hayo kuelekea nyumbani kwao Bukoba mkoani Kagera.

Amesema chanzo cha mauaji hayo kinadaiwa ni wivu wa mapenzi, ambapo Prudence alikuwa akimtuhumu Petronel kuwa na uhusiano na Mwanaume mwingine ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), ambaye pia anadaiwa kumpa ujauzito.

Mwili wa Petronel unaagwa hii leo chuoni hapo na Kamanda Bwire amesema kuwa mara baada ya mwili huo kuagwa, utasafirishwa kwenda nyumbani kwao Sumbawanga mkoani Rukwa kwa ajili ya mazishi.

Rais TFF awatumia ujumbe mashabiki Young Africans
Manji mikononi mwa TAKUKURU, sababu za kushikiliwa hizi hapa