Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) nchini Kenya, Brian Kibet Bera, amenusurika kifo baada ya kupigwa risasi ya bega la kushoto na walinzi wa Ikulu ya Kenya.

Mwanafunzi huyo amelazwa katika katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta baada ya kupigwa risasi na polisi kwa kung’ang’ania kuingia Ikulu ya Nairobi kinyume cha sheria.

Kwa mujibu wa msemaji wa Ikulu ya Kenya, Kanze Dena-Mararo amesema kuwa tukio hilo lilitokea Jumatatu na mshukiwa alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Kileleshwa na kusajiliwa katika Kitabu cha Matukio nambari 39 kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kwa matibabu.

”Tunachukua fursa hii kukumbusha umma kwamba Ikulu ni mahali palipotengwa kuwa chini ya ulinzi mkali kwa mujibu wa Sheria ya Maeneo Yanayolindwa (Protected Areas Act). Kwa sababu hiyo, hakuna mtu yeyote anayeruhusiwa kuingia Ikulu pasipo na ruhusa ya mamlaka yenye jukumu hilo.” amesema Kanze.

Aidha, amesema kuwa kwasasa uchunguzi unaendelea kubaini nia ya mtuhumiwa huyo ya kutaka kuingia Ikulu kinyume cha sheria ili hatua stahiki zichukuliwe baada ya uchunguzi kukamilika.

Hata hivyo, tukio hilo limezua mjadala mkali katika mitandao ya kijamii nchini Kenya huku baadhi watu wakihoji kwanini mwanafunzi huyo aliamua kuchukua hatua hiyo.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Juni 12, 2019
Je unatafuta ajira?, Hizi hapa nafasi 10 za ajira kwa ajili yako