Katika hali isiyotarajiwa, mwandishi wa habari mmoja kutoka Marekani amepata umaarufu ghafla nchini Kenya kufuatia kutokea kwa hitilafu ya umeme katika maeneo mengi ya nchi siku ya Jumanne, Januari 11, 2022.

Mwanahabari huyo, Ben Terry wa shirika la utangazaji la KPLC 7 TV lililoko katika jimbo la Louisiana aliingizwa kwenye siasa za kukatika kwa umeme na wakenya waliokuwa na hasira ambao walitaka majibu kutoka kwa kampuni ya Kenya Power.

Terry alijikuta pabaya huku Wakenya wengi wakimiminika kwenye ukurasa wake wakimtaka aeleze hali ilivyo na hatua zilizochukuliwa na kampuni hiyo kuhusu tatizo la kupotea kwa umeme mara kwa mara.

Hilo lilichochewa na jina lake la mtandao wa kijamii, KPLC, ambalo ni mfano wa Kenya Power ambapo kutokana na hivyo, wakenya wengi kwenye mitandao ya kijamii walijikuta wamejichanganya kwenye Twitter kuhusina na jina lake la KPLC na lile la kampuni ya kusambaza umeme nchini Kenya.

Mwanahabari huyo, alieleza kuwa mkanganyiko huo ulikuwa baraka kwani alipata wafuasi kadhaa mitandaoni nchini Kenya kutokana na kisa hicho. “Nimepata wafuasi kadhaa Twitter kutoka Kenya katika muda wa saa 24 zilizopita. Kwa taarifa yenu, sihusiani na KPLC ambayo ni Kenya Power and Light Company kwa vyovyote vile. Hata hivyo, ninatumai mtapenda kufurahia habari za hali ya hewa Kusini Magharibi mwa Louisiana. Karibuni!” alifafanua.

Mwanahabari huyo alieleza zaidi kuwa hana mpango wa kuinunua kampuni ya Kenya Power baada ya kuulizwa na mmoja wa wafuasi wake wapya kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uhusiano wake na kampuni hiyo.

“La hasha! natamani sana ningekuwa na uwezo wa kukusaidia lakini sina nia ya kununua kampuni ya umeme.” Alimjibu.

Ili kuwapa matumaini Wakenya walioathiriwa na hitilafu hiyo ya umeme, Terry alibainisha kuwa wakati fulani alilazimika kukaa kwa wiki moja bila umeme baada ya jimbo lake kukumbwa na kimbunga.

“Nguvu zetu zilikatika kwa wiki moja huko Louisiana baada ya Kimbunga Laura. Tunatumai, (nguvu za umeme) zitarejeshwa hivi karibuni nchini Kenya!” Alisema.

Hitilafu tatu kuu za usambazaji umeme ziliingiza Kenya katika giza kufuatuia kukatika kwa umeme nchini kote katika miaka ya hivi karibuni siku chache tu baada ya kutangazwa kupunguzwa kwa gharama ya umeme kwa asilimia 15.

Kampuni ya Kenya Power ilibainisha kuwa hitilafu hiyo ya asubuhi ilitokea baada ya minara inayotumia njia ya umeme yenye nguvu ya juu inayounganisha Nairobi na bwawa la kuzalisha umeme la Kiambere kuporomoka mwendo wa saa nne Jumanne, Januari 11.

Kufikia saa kumi na moja jioni Kenya Power ilikuwa imerejesha umeme katika maeneo mengi ya nchi isipokuwa Kitui, Mwingi na Garissa. Hata hivyo, hitilafu ya tatu iliripotiwa na kuathiri sehemu za katikati mwa jiji la Nairobi, Kilimani, Hurlingham, Syokimau, Athi River, Kitengela, Mlolongo na maeneo ya karibu.

Nape atema cheche kwa wamiliki wa vyombo vya habari
Raila kuanza kampeni za kuingia Ikulu katika Ngome ya Kenyata.