Mwanamke mmoja wa jijini Glasgow nchini Scotland amepata majeraha ya jicho baada ya kutumia kimakosa dawa ya kusaidia kuongeza nguvu za kiume badala ya dawa ya kutibu macho.

Hatua hiyo imetokana na kosa la mtoa dawa kushindwa kusoma kwa usahihi mwandiko wa daktari, kutokana na uhalisia wa namna ambavyo miandiko ya madaktari huwa ya ‘kuchoronga’ na kusababisha kusomeka kwa shida.

Dawa iliyokusudiwa na daktari kwa tiba ya macho ni dawa ya kupaka ya VitA-POS, lakini mtoa dawa alisoma vibaya na kumpa mgonjwa dawa aina ya ‘Vitaros cream’.

‘Vitaros cream’ ni dawa inayotumika kusaidia wanaume wenye tatizo la kusimamisha uume vizuri wakati wa tendo la ndoa, na hupakwa kwa tahadhari baada ya mhusika kupimwa na kupewa maelekezo stahiki na daktari.

Tukio hilo limeripotiwa katika jarida la BMJ Case Reports toleo la Desemba, ambapo wataalam wa jarida hilo wameshauri madaktari kutumia mwandiko mkubwa ili kuepuka makosa ya usomaji wa miandiko ya mkono.

Imeripotiwa kuwa mwanamke huyo aliyepata majeraha ya macho aliwahishwa hospitalini. Wataalam wa macho walimsaidia na alipona baada ya siku kadhaa.

Dkt. Magdalena Edington wa chuo cha tiba kiitwacho Tennent Institute of Ophthalmology cha jijini Glasgow aliandika kwenye jarida la BMJ Case Reports akionesha kushangazwa na namna hali hiyo ilivyotokea.

“Kukosea kwa kuchanganya maandishi ni jambo la kawaida, na majina ya dawa zenye mfanano inaongeza mkanganyiko zaidi,” aliandika Dkt. Edington.

“Hata hivyo, inashangaza kuona kuwa hakuna hata mtaalam mmoja ikiwa ni pamoja na mgonjwa mwenyewe, ambaye alijiuliza inakuaje dawa za kusaidia uume apewe mgonjwa ambaye ni mwanamke!?” Aliongeza.

Mtaalam huyo alifafanua kuwa wameona ni muhimu kuliweka suala hilo kwenye jarida hilo maarufu ili kusaidia kutoa elimu kwa wengi kuwa makini zaidi wanapotoa dawa kwa wagonjwa.

Video: Huu ni uwekezaji mkubwa, ni lazima nchi ipate mapato- Dkt. Chegeni
JPM asema Changamoto zitakazoshindikana awamu hii hazitatatuliwa mbeleni

Comments

comments