Mwanamke wa Marekani ameweka historia na kuvunja mwiko baada ya kuwa mwanamke wa kwanza kuhitimu mafunzo ya kikosi maalum cha ‘Marine’ nchini humo ambayo yana uwiano na sehemu ya mafunzo ya ukomando yaliyojikita katika mapambano ya ardhini.

Mwanamke huyo ambaye hakupenda jina lake litajwe, amehitimu mafunzo hayo Jumatatu katika eneo la Quantico, Virginia.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Jeshi la Marekani, mwanamke huyo amepewa kazi ya kwanza ya kuongoza vikosi 40 vya jeshi vyenye nguvu.

Kamanda wa vikosi maalum vya jeshi la Marekani, Jenerali Robert Neller ametweet picha ya mwanamke huyo na kueleza kuwa anajivunia kuwa naye pamoja na viongozi wenzake.

Kwa mujibu wa BBC, kati ya wanajeshi 131 walioshiriki mafunzo hayo maalum, ni wanajeshi 88 pekee waliohitimu. Asilimia 10 ya wanajeshi wanaopangiwa mafunzo hayo hushindwa katika siku ya kwanza.

Machi 2016, aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama alifungua milango ya nafasi za jeshi kwa wanawake na kutaka wapewe nafasi hata kwenye vikosi maalum vya juu.

Hata hivyo, utafiti uliofanywa ulionesha kuwa wanajeshi wengi wa Marekani wanapinga wanawake kujumuishwa kwenye oparesheni za vikosi maalum.

Safaricom yajibu tuhuma za kushiriki uchakachuaji matokeo Kenya
Takukuru yawafungulia mlango Lema, Nassari