Kampuni ya Tanzania Pharmaceuticals Industries (TPI) imeburuzwa mahakamani kwa madai ya kuiuzia Bohari ya Dawa (MSD) dawa za kupunguza makali ya Virusi Vya Ukimwi (ARVs) zisizokidhi viwango vya ubora.

Mwanasheria Mwandamizi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Shadrack Kimaro, Ijumaa iliyopita aliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam kuwa dawa hizo zilikuwa na nembo ya kutengenezwa Machi 2011 na kuisha muda wake 2013 ziliwasilishwa kwa MSD Aprili 5 na Aprili 11 mwaka 2011.

Katika kesi hiyo, washitakiwa ni pamoja na Shango ambaye ni Mhasibu msaidizi wa TPI, Seif Salum Shamte ambaye ni Mkurugenzi wa TPI na Alfred Msoffe, Mkurenzi Mtendaji wa kampuni hiyo.

Ameeleza kuwa bidhaa hizo zilizowasilisilishwa zilipokelewa na maafisa wa MSD na kuthibitishwa kuwa zinakidhi viwango. Hivyo, MSD iliwalipa TPI mara mbili kwa njia ya hundi. Hundi ya kwanza ilikuwa ya shilingi 94,153,674.24 na ya pili shilingi 54,196,482.24.

Msoffe na Mulimila walipokea hundi hizo kwa niaba ya TPI na kuziweka katika akaunti ya kampuni hiyo katika benki ya CRDB tawi la Holland.

Aidha, ilidaiwa kuwa fedha hizo zilitolewa baadaye na Shamte pamoja na Shango huku aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Kanda ya Dar es Salaam, Madabida, akifahamu kilichokuwa kikifanyika.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa baada ya MSD kusambaza dawa hizo kwenye matawi yake ya kanda za Iringa, Tanga, mwanza na Mwanza, ilipata taarifa na matukio yanayoashiria kuwa bidhaa hizo hazikukidhi viwango. Hivyo, MSD iliiomba Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kufanya uchunguzi katika maeneo hayo.

Kimaro alisema kuwa baada ya uchunguzi uliofanyika Agosti 2012, TFDA ilibaini kuwa dawa hizo hazikuwa na viwango vinavyotakiwa kwa ajili ya matumizi yaliyokusudiwa na kwamba zilikuwa tofauti na zilizokuwa zimekaguliwa awali.

“Uchunguzi wa sampuli ulibaini kuwa dawa zilizowasilishwa na kusambazwa hazikuwa zinakidhi viwango na zilikuwa tofauti na zile ambazo TFDA ilizikagua na kuzipitisha awali,” alisema Kimaro.

Alisema kuwa MSD ililazimika kuondoa dawa hizo katika hospitali zote zilizokuwa zimepelekewa.

Baada ya kuwasilisha, washtakiwa wote walikana mashtaka dhidi yao. Hakimu aliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 17 mwaka huu.

TRA yaagiza biashara zote zilizofungwa zifunguliwe
DR Congo yataja kikosi cha maangamizi dhidi ya Taifa Stars

Comments

comments