Vyama vya siasa nchini vimetakiwa kutumia haki zao za kikatiba kwa hekima na busara ili waweze kufaidi haki waliyopewa na kuacha kuchukua hatua za ubabe na kutishia hali itakayopelekea vyombo vya dola nchini kuchukua hatua kwani ni viashiria vya uvunjifu wa amani.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. George Masaju alipokuwa akitoa wito kwa wananchi na wanasiasa nchini kuhusu masuala ya utii wa sheria na kudumisha amani nchini kupitia mkutano na vyombo vya habari leo Jijini Dar es Salaam.

Mhe. Masaju alisema kuwa kumekuwa na baadhi ya wanasiasa wanaotoa vitisho vya ufanyaji wa mikutano kinyume na taratibu za kisheria kwa kisingizo cha uvunjaji wa haki za kikatiba jambo amablo sio kweli.

“Napenda kuvishauri vyama vya siasa nchini kuacha kutumia kauli za kibabe na vitisho na kuzitumia haki zao za kikatiba kwa hekima na busara, hali itakayopelekea vyombo vya dola nchini kuchukua hatua kwani ni viashiria vya uvunjifu wa amani”.

“Wanasiasa wawe wakweli na kuacha kupotosha watu kwamba wamenyimwa haki ya kikatiba ya kufanya mikutano kwani wapo baadhi yao wanaofanya mikutano katika majimbo yao baada ya Jeshi la Polisi kujidhirisha kwamba kutakuwa hali ya amani na utulivu”. Alisema Mhe. Masaju.

Aidha, Mhe. Masaju alipongeza juhudi zinazofanywa na viongozi mbalimbali wa dini nchini kwa jitihada wanazofanya za kushauri katika kufika muafaka wa hali ya kisiasa nchini na kuwashauri kuhubiri amani na utulivu kwa waumini wao.

Akitoa ufafanuzi wa tamko la baadhi ya vyama vya upinzani kutaka  serikali kuvifuta vyama hivyo Mhe. Masaju alisema kuwa suala hilo ni kinyume na katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania kwasababu katiba hiyo inaruhusu mfumo wa vyama vingi.

“Katiba ya jamhuri ya muungano wa Tanzania inaruhusu mfumo wa vyama vingi hivyo kama serikali haiwezi kuvifuta kwasababu itakuwa ni kinyume cha katiba inayoiongoza nchi na pia sidhani kama tamko hilo limetolewa na vyama vyote vya upinzani ila ni namna ya wao kufanya siasa kuhisi”. Alisema Masaju

Vyombo Vya Sheria Vyatakiwa Kuwasaidia Watumiaji Madawa Ya Kulevya
Bodi Ya Filamu Kuendeleza Ushirikiano Na Wadau