Mwandishi wa habari wa Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW) kutoka Zanzibar ambaye pia ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Salma Said amesimulia vipigo na vitisho alivyopokea kutoka kwa watekaji wake.

Akiongea jana mbele ya waandishi wa habari katika ofisi za Baraza la Habari Tanzania (MCT) baada ya kutoka hospitali alikokuwa akipatiwa matibabu na baadae kituo cha polisi alipokuwa akihojiwa, Bi. Salma alieleza kuwa alipofika katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokeo Zanzibar, Ijumaa ya Machi 18 ilimbidi akae sehemu kumsubiri dereva wake aliyekuwa akimfuata uwanjani hapo.

Salma Said akionesha wana habari dawa alizopewa hospitalini

Salma Said akionesha wana habari dawa alizopewa hospitalini

Alisema ghafla walikuja watu wawili asiowafahamu wakamkamata na kumuingiza kwenye gari lao wakiwa wamemfunga ushungi wake usoni ili asione wanapoelekea. Bi. Salma alisema kuwa walimpeleka kwenye chumba kimoja chenye vitambaa vingi na hapo walifunua nyuso zao akawaona.

“Mmoja alikuwa na kovu shavuni, mrefu na mwingine mweupe kidogo, waliniweka kule ndani bila kupata chakula chochote,” alisimulia.

Alisema kuwa watu hao walimtesa na kumpiga ngumi na mateke huku wakimpa vitisho vikali kutokana na namna alivyokuwa akiripoti habari za uchaguzi wa Zanzibar na kisha waliahidi kumuachia baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa marudio visiwani humo na mgombea wa CCM kutangazwa mshindi.

Katika mkutano huo na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), viongozi wa MCT walihudhuria pia na kupinga vikali utekaji na utesi huo dhidi ya mwanahabari.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, alisema kuwa jeshi lake linaendelea kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo, hivyo hayuko kwenye nafasi nzuri ya kutolea majibu wakati huu.

 

Mkuu wa Wilaya amuomba Magufuli amuondoe
Magufuli: Wana CCM tusilazimishe Mambo Umeya Dar