Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) ametoa onyo kali kwa Mweka Hazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Issa Mbilu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Fedha na Biashara wa Halmashauri hiyo kwa kutotekeleza majukumu yake ipasavyo na kumtaka kuacha kiburi.

Onyo hilo amelitoa wilayani Korogwe wakati wa kikao kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe na Halmashauri ya Mji wa Korogwe chenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kukagua miradi ya TASAF na kujiridhisha na utekelezaji wake.

Dkt. Mwanjelwa amemtaka Mweka Hazina huyo, kutokuwa kikwazo kwenye malipo halali ya watumishi wenzie pamoja na kutoa sababu zenye mashiko za kukataa kuidhinisha malipo ya watumishi kwa maandishi pindi anapobaini mapungufu.

Aidha, amemsisitiza Mweka Hazina huyo kuacha kuipendelea idara yake katika kulipa stahili mbalimbali ikiwamo posho ya saa za ziada kazini na kuongeza kuwa malipo ya posho hiyo sio kwa ajili ya watumishi wa Idara ya Fedha na Biashara pekee bali ni kwa ajili ya watumishi wote.

Hata hivyo, Dkt. Mwanjelwa amewataka watumishi wa halmashauri hizo kutofanya udanganyifu ili wapate malipo yasiyostahili kwani ni kosa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za utumishi wa umma na kusisitiza kuwa kila mtumishi afanye kazi kwa bidii ili alipwe anachostahili.

 

Video: Fahamu watu maarufu wanaotumia mashoto na tabia zao
Adaiwa kumuua mpenzi wake na kumtundika kwenye nyaya za umeme