Mkoa wa Tabora umeanisha maeneo ya vipaumbe vya uwekezaji katika kila Halmashauri nane za Mkoa huo ambayo yatajengwa viwanda vikubwa na uanzishaji wa ranchi kwa ajili ya ufugaji wa ng’ombe.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri wakati wa majumuisho ya kikao cha Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji mkoani humo.

Amesema kuwa upande wa Wilaya ya Urambo wamepewa jukumu la kutenga eneo la ujenzi wa Kiwanda cha Kusindika Tumbaku, Halmashauri ya Kaliua wamepewa jukumu la kujenga kiwanda cha mazao ya Misitu.

Mwanri ameongeza kuwa Sikonge wenyewe wanatakiwa kuandaa eneo kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki ikiwemo asali na nta kwa ajili ya kuongeza ubora wake ili yaweze kupata soko kubwa ndani na nje ya nchi.

Aidha, Mwanri alisema Igunga wamepewa jukumu la kuimarisha kilimo kikubwa cha pamba kwa ajili ya viwanda Tabora na Manonga na kuongeza maeneo ya miradi ya umwagiliaji mpunga, ujenzi wa viwanda vya kukoboa mpunga ambavyo vitasaidia kuuweka katika madaraja.

Hata hivyo, amesema kuwa Uyui watahusika zaidi kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti na mazao mengine.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa Manispaa ya Tabora wanatakiwa kutenga eneo kwa ajili ya ukanda maalumu wa uwekezaji ambapo vitajengwa viwanda kama vile wa EPZA Ubungo  Jijini Dar es salaam.

Video: Waziri Mkuu azindua kampeni ya siku 16 kupinga ukatili wa kijinsia
Ziwa Victoria lazidi kuwa hatari, wengine 14 wafa maji